THBUB yaitaka jamii kuacha mitazamo potofu kwa walemavu

0

NA DOTTO KWILASA, DODOMA

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imewataka wananchi kuachana na imani ,mila,desturi na mitazamo potofu  inayo wafanya watu wenye ulemavu kuvunjika moyo na kujiona hawakubaliki katika jamii.

Aidha baadhi ya mila hizo potofu zilizo jengeka na kuota mizizi miongoni mwa wanajamii zinawanyong’onyeza Wenye ulemavu na kujiona hawawezi na hawana mchango wowote kwa jamii  na Taifa kwa ujumla katika shughuli zinazohusu maendeleo.

Hayo yamezungumzwa  jana  jijini hapa na Mwenyekiti wa THBUB  Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alipokuwa wakati akitoa tamko  wakati wa Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu.

Katika maadhimisho hayo alisema “Pamoja na pongezi hizo kwa Serikali,Tume inatambua juu ya kuwepo watu wenye ulemavu unaoonekana na usioonekana,aidha Tume inatambua kwamba watu wenye ulemavu bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kiafya,elimu,ajira,unyanyapaa na unyanyasaji,”alisema Mwaimu na kuongeza;

“Kwa muktadha huo Tume inatoa rai kwa Serikali kuendeleza juhudi za makusudi katika kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanawekeza mazingira mazuri ya kupata mahitaji yao kulingana na hali zao za ulemavu unaowakabili,”alisema mwaimu.

Aidha alisema kuwa Tume inawataka wananchi wanaoishi na watu wenye ulemavu kuchukua hatua za kuwasaidia na kuwaona kuwa sehemu yao.

Aliongeza kuwa kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu Tume inawasihi wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya zao ili kuweza kubaini mapungufu waliyonayo katika viungo vya miili yao na kuchukua hatua stahiki ili kuzuia ulemavu unaoweza kuzuilika.

Pamoja na Mambo mengine alisema THBUB inaiomba Serikali kuwatumia vyema wataalamu wake kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na ulemavu usioonekana ambapo athari zake zinaweza kumuathiri mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla.

Aidha Tume inaahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa, zinakuwa na kutetewa hapa Nchini.

“Tume ya haki za binadamu na Utawala bora kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutetea haki za watu wenye ulemavu na kuweka msukumo wa utekelezaji wa sheria ya watu wenye ulemavu Na. 9/2010 na miongozo ya haki kimataifa na kikanda, “alisema Mwenyekiti.

Chimbuko la siku ya watu wenye ulemavu linatokana na Azimio la Baraza kuu la Umoja wa Mataifa Na. 47/3,la 1992 ambalo lilipitisha siku ya Desemba 3 ya kila mwaka kuwa ni siku ya ya maadhimisho ya watu wenye ulemavu Duniani,

Lengo la Maadhimisho haya ni kuhamasisha jamii katika Nchi husika kutambua,kuheshimu na kutetea haki na fursa sawa,ushiriki wa watu wenye ulemavu katika masuala ya maendeleo,mahitaji yao,kutafakari changamoto zinazowakabili na kutafuta namna ya kukabiliana nazo.

Tume ya haki za Binadamu na Utawala bora (THBUB) inaungana na wadau wote wa haki za watu wenye ulemavu duniani katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu ikiwa na kauli mbiu “si kila ulemavu unaonekana”.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here