Teknolojia yasaidia kutokomeza ujangili wa Faru

0

NA JONAS MUSHI, DODOMA

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limesema kuwa matumizi ya teknolojia ni miongoni mwa sababu za kutokomeza ujangili wa Faru kwa miaka mitatu mfululizo.

Mratibu wa Faru nchini na Ofisa Mwandamizi wa TANAPA, Philbert Ngoti, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dodoma wakati akiwasilisha mada ya mpango wa uhifadhi wa wanyama waliohatarini kutoweka, wakati wa mkutano na wahariri na waandishi wa habari waandamizi wanaoandika habari za uhifadhi na utalii.

Ngoti alisema katika kipindi hicho hakuna kifo cha faru hata kimoja kilichotokana na ujangili kutokana na kuwafungia faru wote vifaa maalumu vinavyotuma taarifa za mahali walipo na hivyo kurahisisha shughuli za kuwalinda dhidi ya ujangili.

Alisema tofauti na awali kabla ya uwepo wa vifaa hivyo walikuwa wakizunguka porini bila kujua maeneo mahususi walipo ili kuimarisha ulinzi.

“Sasa hivi ukienda eneo ambalo kuna faru ndipo utakapokuta askari wengi wa doria lakini zamani mnaweza kuwa hapa lakini faru wapo eneo jingine wakishambuliwa na majangili hadi mje mfike eneo walipo unakuta wameshakimbia,” alisema Ngoti.

Hatua hiyo imewezesha kulinda faru na kusaidia kuongeza idadi yao kutoka faru 161 mwaka 2018 hadi faru 190 Machi 2020.

Alisema vifaa hivyo vinatumia teknolojia ya Habari na Mawasiliano na husimikwa katika mwili wa faru na kutuma taarifa katika minara ya mawasiliano na kisa katika kompyuta zinazoonyesha eno alipo.

Alisema mradi huo ni miongoni mwa shughuli zinazofanywa katika utekelezaji wa Mkakati wa Kuhifadhi Faru wa Mwaka 2019-2023 ukiwa na lengo la kufikisha faru 205.

Mbali na ufungaji wa vifaa hivyo Ngoti alisema Mkakati huo una shughuli zingine za uhifadhi wa tembo zipatazo 143.

Faru ni miongoni mwa wanyama walio hatarini zaidi kutoweka duniani kutokana na ujangili wa pembe zao ambazo zina soko nchini China na Tailand.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya faru walipotea duniani na kwamba Tanzania miaka ya 1970 walikuwa 10,000 ikiwa nchi yenye faru wengi, ambao walipungua hadi kufika 15 miaka ya 90 kutokana na ujangili.

Alisema hadi Machi mwaka huu, kulikuwa na faru 190 ambao wapo katika Hifadhi ya Taifa Mkomanzi na Great Serengeti Ecosystm inayobeba Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi eneo la Ngorongoro, mapori ya Ikorongo, Maswa na Hifadhi ya Taifa ya Masai Mara nchini Kenya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here