TCRA anzeni na kero hizi matumizi ya simu

0

Hivi karibuni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile alitoa miezi mitatu kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) kumaliza kero katika sekta hiyo zikiwamo nyingi zikiwa zinazohusiana na vifurushi vya simu.

Tunaungana na Waziri kusisitiza umuhimu wa kuzifanyia kazi haraka kero hizo ambazo zimedumu kwa muda mrefu licha ya kuwepo kwa sheria na miongozo inayozibana kampuni za simu kufanya baadhi ya mambo.

Pamoja na kuwepo kwa mwongozo wa kuwasilisha malalamiko TCRA lakini wanannchi wengi hawaufahamu hivyo kampuni za simu zinatumia mwanya huyo kufanya mambo kinyume cha kanuni.

Mwongozo pia ni mrefu kwani unamtaka mtumiaji wa huduma hizo kuwasilisha kwanza malalamiko yake kwa kampuni ya simu husika na asiporidhika ayawasilishe TCRA, kisha kamati ya malalamiko ya TCRA na hatimaye katika Baraza la Uamuzi wa Haki.

Miongoni mwa kero zinazozungumzwa na watumiaji wengi wa simu za mkononi ni wingi wa matangazo kutoka namba binafsi na namba maalum. Matangazo haya yanatumwa kwa mtumiaji pasipo idhini yake yakimtaka ashiriki jambo fulani ikiwemo michezo ya kubashiri.

Pia kero kubwa ambayo inasumbua wengi ni mfumo wa kupewa muda maalumu wa kutumia vifurushi utakavyonunua hivyo hata kama haujatumia kifurushi chako, muda utakapokwisha hutoweza kutumia huduma hiyo licha ya kwamba umekwisha ilipia.

Pia kuna uwepo wa vifurushi ambavyo ni kama utapeli hasa pale mtumiaji anapogawanyiwa muda wa kutumia vifurushi ambapo vifurushi vya kutumia usiku huwa ni vikubwa kuliko vile vya kutumia mchana. Inafahamika kuwa watu wengi usiku wanakuwa wamepumzika hivyo ni nadra sana kukuta mtu anaongea na simu usiku kuliko mchana.

Nyingine ni miamala kutofika kwa wakati kwa wahusika na usipochukua hatua ya kufuatilia fedha hiyo hairejeshwi. Hii ipo pia kwenye kununua vifurushi ambapo unaweza kununua kifurushi kutoka akaunti ya simu yako, unakatwa fedha kwenye akaunti lakini hupokei kifurushi wala ujumbe wa kucheleweshewa na usipopiga simu huduma kwa wateja fedha yako hairudishwi.

Hizi ni miongoni mwa changamoto ambazo TCRA wakianza nazo watakuwa wametatua ero kubwa kwa watumiaji wa simu nchini.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here