TBA ilivyotekeleza miradi 85 ya Bil. 142 miaka mitano

0

NA MWANDISHI WETU

Imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka mitano Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), umefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa Majengo ya Serikali 85 nchi nzima yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 142 ikiwamo miradi ya “Buni – Jenga”.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Elius Mwakalinga, ameyasema hayo jjini Dodoma wakati akifungua mkutano wa mwaka wa 2020/2021  wa  Baraza la Wafanyakazi wa wakala huo na kusisitiza kuwa hiyo ni hatua kubwa kitaasisi japo hatua hiyo haijawaondoa moja kwa moja kwenye changamoto za kuchelewa kwa baadhi ya miradi ya ujenzi.

Mwakalinga aliutaka uongozi wa wakala  kutazama kwa undani hatua gani walizofikia katika utekelezaji wa majukumu yao hususani namna wanavyoweza kushughulikia changamoto  katika kila eneo la kiutendaji.

“Hakikisheni mnajitathimini kwa kina bado kuna changamoto za kuzifanyia kazi na Serikali yenu inawaamini katika utoaji ushauri na usimamizi wa miradi ya ujenzi na usimamizi wa miliki za Serikali”, alisema Katibu Mkuu huyo.

Aidha, aliupongeza Wakala kwa hatua nzuri waliyofikia katika miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwamo ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Saalam ambapo hapo awali kulikuwa na malalamiko mengi.

Mwakalinga aliitaka TBA kuendelea kujali masuala ya wafanyakazi kutoka sekta binafsi kwa kuzingatia kuajiri watu wengi kwenye miradi ya ujenzi hususani walinzi, babalishe, mamalishe, watalaamu wa ujenzi, mafundi, vibarua na wanafunzi wa taaluma zote kutoka vyuo vikuu ili kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na kupunguza umaskini nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala  huo, Daud Kondoro, alimueleza Mgeni rasmi kuwa katika mkutano huo wajumbe wa baraza la wafanyakazi watapewa elimu ya “haki za mtumishi mahali pa kazi na wajibu wa mtumishi kwa mwajiri” ili iweze kuwasadia kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here