Na Dotto Kwilasa, DODOMA
Mamlaka ya usimamizi wa wanyama pori hapa nchini (TAWA) imeanza rasmi ufunguzi wa mabucha ya nyama yatakayokuwa yakiuza nyama ya wanyamapori hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kufungua bucha ya kwanza ya kuuza nyama hiyo Jijini , Mwenyekiti wa bodi ya TAWA, Meja Jenerali Msitaafu Hamis Semfuko amesema hatua hiyo ni kutimiza maagizo yaliyotolewa na Rais Dk. John Magufuli kuwa wananchi waanze kunufaika na nyamapori.
“Nimekuja hapa na wajumbe wenzangu kwenye ufunguzi wa bucha la kwanza hapa nchini kuuza nyamapori na hili ni agizo la Rais Magufuli kuwa tuhakikishe wananchi wananufaika na rasilimali zao ikiwamo hizi nyamapori” amesema

Jenerali Semfuko alibainisha kuwa wanyamapori watapatikana kwa njia ya vibali maalum vya uwindaji,kwa wawindaji wa kitalii na kwa wananchi wenyewe watakaoanzisha ranchi za kufuga wanyamapori ambapo ameahidi kuwa TAWA ipo tayari kuwapatia Mitamba ya uanzishaji ufugaji wanyamapori.
Pia, alibainisha kuwa mabucha ya wanyamapori yatapatikana katika maeneo mbalimbali nchini huku ujangili wa wanyama utaendelea kuthibitiwa na usafi utazingatiwa na kwamba utaratibu wa uanzishaji wa mabucha ya wanyamapori upo wazi kuanzia hivi sasa .
Kwa upande wake Kaimu Kamishna TAWA, Mabula Nyanda amesema bucha la nyama pori lililozinduliwa limetokana na wanyama waliowindwa huku akitoa wito kuwa ukitaka kula nyama hiyo lazima uijue TAWA kwani ndio msimamizi mkuu wa wanyamapori katika masuala ya uvunaji.
“Ukijifunza na kuielewa TAWA itasaidia kuwa wazalendo na kuepuka uwindaji haramu unaoisababishia hasara Serikali,” alisema.

Kutokana na hayo baadhi ya wananchi wa Mtaa Kishoka kata ya Chang’ombe jijini hapa Walipata nafasi ya kuzungumza hatua hiyo na kusema kuwa ni ya kizalendo .
Mwenyekiti wa mtaa huo, Juma Maulid alisema kuanzishwa kwa bucha la nyamapori mbali na kuwarahisishia wananchi kupata nyama kiurahisi ni njia mojawapo ya kuwaenzi watanzania kwani kwa muda mrefu hawajawahi kupewa nafasi ya kutumia rasilimali zao .
“Kuna watanzania ambao tangu wamezaliwa wengine Wana miaka 40 lakini hawajawahi kula nyama pori Kutokana na mifumo iliyokuwepo,tunaishukuru serikali kwa kutuona,tulikuwa tunapitwa sana,”alisisitiza.
