Tanapa yapewa tuzo ya ubora wa huduma

0

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Jumuiya ya Ulaya inayojihusisha na utafiti wa ubora imetoa tuzo ya dhahabu ya ubora wa huduma kwa mwaka 2020 kwa Shirika la Hifadhi ya Taifa Tanzania (Tanapa).

 Tuzo ya huduma za viwango hutolewa kila mwaka na taasisi ya European Society for Quality Reseach (ESQR).

Tuzo hiyo itapokelewa rasmi na balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Jestas Nyemanga mjini Brussels, Ubelgiji wiki ijayo na hutolewa kwa ajili ya kutambua taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za viwango vya juu.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Desemba 4, 2020 na kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi,  Pascal Shelutete inaeleza kuwa washindi wa tuzo hizo huchaguliwa kwa kuzingatia matokeo ya kura zilizopigwa na taasisi zilizoshinda awali, maoni ya wateja na utafiti wa masoko.

Aidha mchakato wa utoaji wa tuzo hiyo unajumuisha utafiti wa taarifa mbalimbali za umma, machapisho, maoni chanya ya wateja, miradi ya kijamii, vyuo vikuu pamoja na maonesho.

“Pia ni matokeo ya mikakati ya shirika la hifadhi za taifa nchini katika kuhifadhi rasilimali za hifadhi pamoja na marejesho chanya kutoka kwa wateja wa kitaifa na kimataifa.”

“Utambuzi huu utakuwa chachu ya kuendelea kuongeza jitihada za uhifadhi endelevu wa hifadhi zetu, kutangaza vivutio katika masoko mbalimbali na kuendelea kuboresha huduma za utalii,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Tuzo hiyo ni matarajio kuwa jitihada hizo zitachangia kuongeza idadi ya watalii kufikia malengo ya Serikali ya kuwa na watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025.

“Shirika la hifadhi linaendelea kutoa wito kwa umma na taasisi za kitaifa na kimataifa pamoja na wadau wa maendeleo kuendelea kutoa ushirikiano katika  kuhifadhi rasilimali za taifa na kuunga juhudi za Serikali za kukuza utalii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” inaeleza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here