Takwimu sahihi zimeipaisha Tanzania kiuchumi

0

Na John Mapepele, Singida

TAKWIMU sahihi zilizokusanywa kutoka kwenye sekta mbalimbali za kimkakati za Mifugo, Kilimo na Uvuvi nchini zimeifanya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli kuingia kwenye Nchi za Uchumi wa Kati duniani.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na ujumbe maalum wa kitaifa ulioongozwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk. Anjelina Lutambi wakati  walipokuwa wanakagua zoezi la kitaifa ya ukusanyaji taarifa za kina za Kilimo, Mifugo, ufugaji wa samaki Mkoani Singida ambalo limekamilika  hivi karibuni kwa mafanikio makubwa.

“Madhumuni makuu ya Sensa hii ni kupata taarifa muhimu za kilimo, mifugo na uvuvi
zitakazotumika katika kupanga na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali
ya maendeleo ya sekta katika taifa la Tanzania, na endapo ukusanywaji wa
takwimu utakuwa kwenye ubora unaositahili utasaidia kulifanya taifa kupea
kwenye uchumi wa juu kabisa katika kipindi kifupi kijacho,” alisema D
k. Chuwa.

Alifafanua, taarifa  kwa mfano za magonjwa ya mifugo na mazao zitaisaidia Serikali kuainisha maeneo yanayokabiliwa na visumbufu/magonjwa  ili kuchukua hatua
stahiki na kupanga mipango ya kudhibiti.Pia taarifa kuhusu uzalishaji wa mazao
zitasaidia kujua kiasi cha uzalishaji kwa maeneo husika na kuiwezesha Serikali
kupanga upatikanaji wa masoko na uwezekano wa kuanzisha viwanda vya kusindika
mazao hayo.

Aidha, taarifa kuhusu upatikanaji na matumizi ya ardhi zitatumika kupanga
mipango ya matumizi bora ya ardhi vijijini hivyo zitatumika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

“Kutokana na umuhimu huo na kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia
ya Mwaka 2030, Sekta ya Kilimo ilipewa Lengo la Pili  la Kutokomeza Njaa, Kuwa na Uhakika wa Chakula, Lishe Bora na Kukuza Kilimo Endelevu. Aidha, lengo hilo limesisitiza umuhimu wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao na pia kusisitiza matumizi bora ya ardhi na kurutubisha udongo, ili kuongeza
uwezo wa binadamu kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi na athari zake
yakiwemo majanga mbalimbali kama mafuriko na ukame pamoja na majanga mengine
ikiwemo ndege waharibifu,” alieleza Dk. Chuwa.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk. Anjelina Lutambi, alisema pamoja na faida za jumla ambazo mkulima atakazozipata Sensa hii itamsaidia mtu mmoja mmoja kutatua changamoto mbalimbali katika kilimo,mifugo na uvuvi hasa upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani, upatikanaji wa masoko kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

“Ni muhimu tukafahamu kuwa takwimu sahihi za mifugo, mazao na uvuvi zitasaidia  uchangiaji wa malighafi za  viwanda  vyetu hivyo kukuza uchumi wetu ambao
tunautaka wa viwanda,” alisisitiza Dk. Lutambi.

Naye, Meneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Singida,
Naing’oya Kipuyo ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Singida kwa kusaidia
kufanikisha zoezi hili ambalo limefanyika kwa takribani siku 50 ambapo pia amewapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano wa  kutosha.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here