TAKUKURU yawabana wakandarasi REA II

0
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brig. Jen. John Mbungo akikabidhi kifaa kwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dk. Tito Mwinuka, ikiwa ni ishara ya kukabidhi vifaa vya Sh. Bil 1.2 vilivyookolewa kutoka kwa wakandarasi waliotakiwa kuvirudisha toka mwaka 2017

NA JONAS MUSHI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetoa siku 14 kwa kampuni za ukandarasi zilizotekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini  awamu ya pili, kurudisha kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) vifaa ghafi vyenye thamani ya jumla ya Sh Bilioni 10.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Gen. John Mbungo alisema vifaa ghafi hivyo ni vile ambavyo havikutumika katika utekelezaji wa miradi na kwa mujibu wa mkataba vinatakiwa kurudishwa TANESCO baada ya kumalizika kwa mradi.

Alisema kuna jumla ya wakandarasi 16 ambao wanatakiwa kurudisha vifaa ghafi hivyo kwa TANESCO na wamekaidi kufanya hivyo licha ya kuandikiwa notisi tangu mwaka 2017.

“Natumia hadhira hii kutoa rai kwa Wakandarasi 16 nitakaowataja, ambao walipelekewa notisi na rea tangu mwaka 2017 lakini bado hawajawasilisha vifaa ghafi hivyo katika ofisi za TANESCO kama notisi walizopokea zinavyowataka kufanya. Ninawaagiza kwamba wahakikishe wamerejesha vifaa ghafi hivyo ndani ya siku 14 kuanzia leo,” alisema Brig. Jen. Mbungo.

Aliwataja wakandarasi hao kuwa ni S/N Shandong Taikai Power Engineering Co. Ltd, Angelique International Limited, Derm Electrics (T) Ltd, Lucky Exports (Energy Division), Spencon Services Limited, LTL Projects (PVT) Limited, Namis Corporate Ltd, O K Electrical & Electronics Services Ltd, China Henan International Co corporation Group Co. LTD na China National Electrical Wire & Cable Imp/Expo Corporation.

Wengine ni States Grid Electrical & Technical Works Ltd; M.F  Electrical Engineering Ltd, Power General &TD Limited, DIEYNEM Co Limited na GESAP Electrical Supplies Co. Ltd; CCC International Engineering Nigeria, Sinotec Co. Ltd, STEG International Services, Nakuroi Investments & DERM Electric (T) Limited, Urban and Rural Engineering Services Limited, na MBH Power Limited.

“Wakandarasi hawa kwa pamoja wanatakiwa kurejesha vifaa ghafi vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 10,” alisisitiza na kuongeza;

“TAKUKURU inaahidi kuendelea kutekeleza majukumu yake ya uokoaji wa Mali za Umma na Binafsi mbali na usimamiaji wa mapambano dhidi ya Rushwa nchini ili kuokoa mali zinazopotelea mikononi mwa wananchi wachache wasio wazalendo.

Katika hatua nyingine TAKUKURU ilikabidhi vifaa ghafi vya jumla ya Sh. Bil. 1.2 ambavyo vilikuwa vimepotea zilikuwa zimepotea kwa mbinu mbalimbali ambazo zimefanywa na baadhi ya wananchi wajanja.

Vifaa ghafi hivyo ni pamoja na Transfoma 34 zenye ukubwa tofauti, Mita za LUKU 1,458 na vifaa vyake, Nyaya zenye urefu wa km 70.8 pamoja na vifaa 30 vya umeme (Ready boards) vya aina tofauti tofauti .

Vifaa ghafi tutakavyokabidhi ni kutokana na Operesheni ya uchunguzi wa Miradi ya REA II iliyofanyika katika mkoa wa Iringa.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007, TAKUKURU kupitia Kurugenzi ya uzuiaji rushwa wanalo jukumu la kufuatilia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo nchini ili kujiridhisha iwapo miradi hiyo ilitekelezwa kwa mujibu wa mikataba iliyoingiwa kati ya Wakala wa Nishati vijijini na Wakandarasi waliopata zabuni za kutekeleza miradi hiyo na iwapo thamani ya fedha iliyotumika inaendana na ubora wa utekelezaji wa miradi hiyo.

“Kutokana na sababu hiyo, Miezi mitano iliyopita – Julai 2020, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ilianzisha operesheni kwenye Miradi ya Usambazaji wa Umeme vijijini – Awamu ya pili (REA II) mradi ambao uko chini ya Wakala wa Usambazaji wa Nishati Vijijini (REA). Mpaka sasa operesheni hii imeshafanyika katika mikoa mitano ya Geita, Iringa, Pwani, Morogoro na Kagera,” alisema.

Kwa mujibu wa mikataba kila mkandarasi, ana wajibu wa kurejesha TANESCO vifaa ghafi vya umeme vinavyobaki baada ya mkataba kukamilika.

YALIYOBAINIKA

Katika mikoa mitano iliyofanyiwa kazi – wakandarasi hawakukabidhi TANESCO vifaa ghafi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 4.3 licha ya kukumbushwa mara kwa mara kufanya urejeshaji huo na kupewa notisi ya kufanya hivyo mwaka 2017.

Alisema mali hizo zilipatikana baada ya kutambua na kuhakiki vifaa ghafi vya umeme vilivyotakiwa kurejeshwa kwa mujibu wa mkataba; kuwatambua wakandarasi wa Miradi ya REA II ambao Mikataba waliyotekeleza iliwataka kuwasilisha Vifaa ghafi TANESCO baada ya kuwa wamepewa notisi ya kufanya hivyo tangu mwaka 2017 na  kushirikiana na TANESCO, REA pamoja na Wakandarasi, kuhakikisha kwamba vifaa ghafi vya umeme vinawasilishwa TANESCO vikiwa kwenye ubora.

“Tukio hili ni moja ya kielelezo ambacho kinathibitisha utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli – Mkuu wa Nchi na Jemedari wa mapambano dhidi ya Rushwa nchini ambaye amekuwa akiyatoa si kwa TAKUKURU peke yake bali kwa wananchi wote wanaopenda maendeleo ya Taifa lao,” alisema Mbungo.

Mbungo alimkabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme TANESCO, Dk. Tito Mwinuka pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Bw. Amos William Maganga.

Alibainisha kuwa makabidhiano hayo ni mwendelezo wa operesheni ya kufuatilia uokoaji wa mali za Serikali na kuhakikisha kwamba Miradi ya Maendeleo ya Nishati Umeme iliyopangwa na Serikali inawafikia walengwa wote na kwa wakati bila kugubikwa na vitendo vya rushwa au ubadhirifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here