Taasis za serikali zahimizwa kutumia NIDC kuhifadhi taarifa zao

0

Na Prisca Ulomi, WMTH

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile amehimiza taasisi za Serikali kutumia Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC) kuhifadhi taarifa zao kwa kuwa ni sehemu salama, ina miundombinu na mifumo ya TEHAMA ya kisasa na ina wataalamu wabobezi na  ina nafasi ya kutosha kwa ajili ya kupangisha mifumo.

Dk. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake yakutembelea NIDC, Dar es Salaam ambapo aliambatana na Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo Mathew, Katibu Mkuu, Dk. Zainab Chaula, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba na watendaji wa Wizara hiyo na kubaini kuwa ni taasisi 84 tu za Serikali zinatumia NIDC kati ya taasisi 149 zinazohifadhi taarifa zake kwenye kituo hicho.

Amezikumbusha taasisi za Serikali kuzingatia agizo la Rais Dk. John Magufuli alilolitoa alipotembelea NIDC kuzindua mfumo wa Kielektroniki wa Kukusanya Mapato (electronic Revenue Collection System – eRCS) mwaka 2017 ambapo umeiwezesha NIDC kuongeza makusanyo ya mapato yake kutoka  shilingi bilioni 1.4 mwaka 2019 na kufikia bilioni  2.76 mwaka 2020.

Naye Naibu Waziri, Mhandisi Kundo Mathew ameipongeza NIDC kwa kutengeneza mifumo mbali mbali ya TEHAMA ambayo inaiwezesha Serikali kuongeza makusanyo ya mapato na kurahisisha maisha kuendana na mahitaji ya wananchi ikiwamo kulipa tiketi ya mabasi kwa njia ya mtandao, kuweka mafuta kwenye gari, kulipa kiingilio kwenye Uwanja wa mpira wa Benjamin Mkapa, usafiri wa kivuko cha Kigamboni, usajili wa leseni BRELA na maegesho yamagari uwanja wa ndege wa Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara hiyo, Dk. Zainab Chaula amewaeleza watendaji wa NIDC washirikiane kwa karibu na wataalamu wa Wizarani Ili kuhakikisha kuwa Serikali inaendelea kuwahudumia Wananchi kwa kutumia TEHAMA ili kuokoa muda waokutafuta huduma za Serikali badala yake watumie kufanyakazi na kuongeza uzalishaji mali.

Meneja wa NIDC, Geofrey Mpangala amesema kuwa watejawanaotumia kituo hicho wamepunguza gharama za uendeshaji na uwekezaji kwenye taasisi zao kwa kuwa hawajengi miundombinu na mifumo ya TEHAMA; wateja wanapata viwango  vya juu vya data yenye kasi na uhakika wa usalamawa data zao na huduma zinatolewa kituoni hapo kwa saa 24.

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba amemshukuru Dk. Ndugulile kwa ziara yake kwa kuwa imeongeza ari na shauku ya utendaji kazi kwa wataalamu wa NIDC ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wateja namifumo ya TEHAMA ili kurahisisha huduma kwa wananchi.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akijadiliana jambo na Meneja wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data, Godfrey Mpangala (wa pili kushoto) wakati wa ziara yake kituoni hapo, Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri, Mhandisi Kundo Mathew na wa tatu kushoto ni Katibu Mkuu, Dk. Zainab Chaula.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here