Sudan kupeleka wanajeshi zaidi Darfur

0

KHARTOUM,SUDAN

Sudan itawapeleka wanajeshi zaidi kusini mwa jimbo lake la Darfur baada ya watu 15 kuuawa katika mapigano ya kikabila.

Shirika la habari la Sudan – SUNA limeripoti kuwa gavana wa jimbo la Darfur Kusini, Musa Mahdi, ametangaza kupelekwa kwa idadi kubwa ya wanajeshi ili kuwasaidia wanaopambana na makabiliano hayo na kukamata silaha.

Mahdi amesema enzi ya mikutano ya maridhiano imeisha na enzi ya utekelezwaji wa sheria imeanza.

 Afisa wa eneo hilo, akinukuliwa na SUNA amesema mgogoro kati ya makabila ya Massalit na Fallata katika eneo la Gereida ulisababisha mapigano ambapo watu wawili wa kabila la Fallata waliuawa.

Fallata kisha wakafanya mashambulizi ya kulipiza kisasi na kusababisha vifo vya watu 13 na kuwajeruhi 34 wa jamii ya Massalit.

 Hayo yanajiri ikiwa ni chini ya wiki moja baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukubaliana kuuondoa ujumbe wa pamoja wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika jimboni Darfur – UNAMID wakati mamlaka yake yatakapomalizika Desemba 31.

Mchakato wa kuwaondoa walinda amani 16,000 utaanza Januari mosi na kukamilika Juni 30.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here