Suala la Chama kama la Morrison

0

NA MWANDISHI WETU

KUNA tetesi kuwa kiungo mchezeshaji raia wa Zambia, Clatous Chama, amekataa mkataba wa miaka miwili Simba wenye dau la Sh Mil. 150 huku watani wao wa jadi wakimtengea Sh. Mil. 300.

Ikumbukwe suala la Bernard Morrison, lilianza tetesi kama hizi na hatimaye matokeo yake yanajulikana.

Kiungo huyo fundi, hivi karibuni ilielezwa amegomea mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kuichezea Simba huku akiwataka viongozi kusubiria hadi mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Hivi karibuni ilielezwa Yanga imeanza mazungumzo ya siri na meneja wa kiungo huyo kwa ajili ya kuhitaji huduma yake msimu ujao baada ya mkataba wake kumalizika Simba.

Taarifa zinaeleza kuwa Yanga imerejea kimyakimya kwa meneja wa kiungo huyo kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya awali ili wafanikishe mipango yao ya kumsajili Chama ambaye ni tegemeo hivi sasa kwenye kikosi  hicho cha Simba.

Kwa mujibu wa taarifa za kimitandao kiungo huyo kabla ya mchezo wa Dar es Salaam Dabi, alifanya kikao na Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya mwisho ya kukamilisha dili hilo la usajili.

Ziliongeza kuwa mabosi wa Simba wamemuwekea kitita cha Sh. Mil. 150 ambacho alitengewa ili asaini na kugoma huku akiomba kuongeza mkataba huo mwishoni mwa msimu.

“Vita kubwa ipo ya kimyakimya kati ya vigogo wa Simba na Yanga ambao wote wanawania saini ya Chama katika msimu ujao, licha ya kuwepo taarifa za kukanusha kuwa nyota huyo anaendelea kubakia Msimbazi.

“Siku moja kabla ya mchezo Dar es Salaam Dabi viongozi wa Simba walifanya kikao na Chama, katika kikao hicho viongozi hao wameonekana kumshawishi kiungo huyo asaini mkataba wa miaka miwili kwa dau la Sh. Mil. 150.

“Wakati Simba wakitaja dau hilo, Yanga wenyewe wanafanya mipango yao kimyakimya ambao wenyewe wapo tayari kumpa Sh. Mil. 300 ili asaini mkataba wa miaka miwili Jangwani,” alisema mtoa taarifa huyo.

Chama alilaumiwa na mashabiki wengi wa Simba kwa kucheza chini ya kiwango katika pambano dhidi ya Yanga Novemba 7.

Mjumbe wa Kamati ya Usajili na Mashindano wa Yanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said hivi karibuni alisikika akisema: “Kama uongozi tupo tayari kusajili mchezaji yeyote atakayependekezwa na kocha.

“Kikubwa hatutaki kumuingilia kocha wetu katika masuala yote yanayohusiana na usajili, hakuna mchezaji tutakayeshindwa kumsajili katika kuelekea usajili wa dirisha dogo.”

Juzi Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Haji Manara, alisema kuwa hakuna suala la Chama kutakiwa na timu yoyote kwa sasa akili zao wanaziweka kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kwa sasa Chama yupo nchini Zambia ambapo amekwenda kwa ajili ya kuitumikia timu ya Taifa ya Zambia maarufu kama Chipolopolo ambayo itacheza leo dhidi ya Botswana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here