Sita jela miaka 20 kwa kuwaingiza raia wa kigeni nchini bila kibali

0

Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo

Mahakama ya wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani imewahukumu kifungo cha miaka 20 Watanzania sita wakazi wa wilaya hiyo kwa kosa la kuwasaidia raia wa kigeni kuingia nchini bila kibali kinyume cha sheria ya uhamiaji.

Mwendesha mashataka wa Idara ya Uhamiaji mkoa wa Pwani Fadhili Festo Msambwa ameiambia mahakama hiyo kwamba watuhumiwa hao wamefanya makosa hayo kati ya tarehe 10 mwezi Oktoba mwaka huu hadi jana asubuhi wakati walipotiwa mbaroni.

Katika kesi hiyo mahakama hiyo pia imewahukumu kwenda jela miaka miwili kila mmoja au kulipa faini ya shilingi laki tano kila mmoja raia 259 toka nchini Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila kibali.

Kesi hiyo ambayo awali ilikuwa isikilizwa katika Mahakama ya wilaya ya Bagamoyo lakini kutokana na wingi wa wahamaiji hao ikahamishiwa kwenye gereza la Kigongoni wilayani humo imehudhuriwa pia na kamishna wa uhamiaji mdhibiti na usimamizi wa mipaka nchini Samweli Mahirane ambaye amesema kufuatia ongezeko la wimbi la uingiaji wa wahamiaji haramu nchini, idara hiyo imeimarisha mkakati wa kudhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu sambamba na kuwachukulia hatua kali mawakala wanaofanya biashara hiyo hususani katika mwambao mwa Bahari ya Hindi.

Kwa upande wake mkuu wa idara ya uhamiaji mkoa wa Pwani Naibu Kamishna wa uhamiaji Paul Eranga ameishukuru mahakama hiyo kwa kutoa adhabu hiyo ambayo amesema itakuwa fundisho kwa watanzania wengine wenye tabia kama hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here