Simba:Ushindi lazima leo

0

NA SHEHE SEMTAWA

WAKATI Mabingwa wa Tanzania Simba wakitarajiwa kuchuka Uwanja wa Taifa wa Zimbabwe, uongozi wa timu hiyo umesema wanaamini kuwa watashinda mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao FC Platinum.

Ikumbukwe mchezo huo unatarajiwa kuchezwa leo, mchezo kuanzia majira ya saa 9:00 kwa saa za Zimbabwe ambapo kwa Tanzania itakuwa saa 10:00 jioni.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili, kutokana na umuhimu wake huku Simba ikiweka wazi kwamba imejipanga kupata matokeo chanya.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema kuwa maandalizi ambayo wameyafanya yanawapa matumaini ya kuweza kupata matokeo ambayo wanayafikiria.

“Kikosi kipo tayari, imara na maandalizi yanakwenda vizuri huku na tunaamini kwamba kwa namna ambavyo tumejipanga tuna nafasi ya kupata matokeo.

“Kikubwa mashabiki wazidi kutuombea na kutupa sapoti ili tuweze kushinda mchezo wetu, benchi la ufundi linatambua kwamba mchezo utakuwa mgumu na wenye ushindani ila tupo tayari,” alisema Barbara.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck alisemakuwa nyota wawili ambao ni John Bocco nahodha wa timu na kipa namba moja Aishi Manulawatakosekana kwenye mchezo huo wa leo.

Vandenbroeck alisema “Tuna masaa machache kabla ya mchezo, tumejaribu kila kitu ili wawe tayari kwa mchezo lakini itakuwa ngumu kuwa tayari.

“John (Bocco) bado yupo kitandani hayupo sawa, Aishi aliumia mchezoi uliopita na anaweza kuchukua wiki au zaidi ili kuwa sawa. Mpaka sasa kuna uwezekano asilimia 50 ya kuwepo kwenye mchezo,”.

Beki wa kulia timu hiyo, Shomari Kapombe, alisema kuwa wanaamini watashinda kwenye mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinun utakaochezwa leo, Uwanja wa taifa wa Zimbabwe.

Simba inayonolewa na Vandenbroeck raia wa Ubelgiji akisaidiana na Seleman Matola ambaye ni mzawa itamenyana na FC Platinum kwenye mchezo wa raundi ya kwanza hatua ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 Kapombe alisema kuwa wana kazi kubwa ya kufanya kwenye mchezo huo ila wanaamini watafanikiwa kwa kuwa wamekubaliana kupambana.

“Wachezaji kwa ujumla tumekubaliana kufanya kazi kwa juhudi kuweza kupata matokeo kwani hakuna kitu kingine ambacho tunakihitaji zaidi ya ushindi ndani ya uwanja.

“Tutakuwa ugenini ila haimaanishi kwamba tutakuwa wageni uwanjani hapana. Hatutakuwa wanyonge tutapambana kwa nguvu kupata matokeo,”alisema Kapombe.

Simba imetinga hatua hii ya kwanza baada ya kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Plateau FC ya Nigeria mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa New Jos Nigeria.

Mchezo wa pili Uwanja wa Mkapa, Simba iliweza kulinda ushindi wake na kufanya dakika 90 kukamilika kwa sare ya bila kufungana.

Mechi zote mbili Kapombe alikuwa ni chaguo la kwanza la Sven ndani ya uwanja.

Aidha, uongozi wa Simba ulisema kuwa kuchelewa kukamilika kwa vibali vya kiungo mkabaji mpya wa Klabu ya Simba raia wa Uganda, Taddeo Lwanga ni sababu kubwa ya nyota huyo kuchelewa kuanza majukumu yake mapya ndani ya Simba.

Lwanga alikamilisha usajili wake na kutambulishwa kujiunga na Simba, Desemba 2, mwaka huu ambapo alianza mara moja mazoezi na kikosi cha mabingwa hao watetezi, mpaka sasa hajacheza mchezo huku kukamilika kwa vibali vyake ikiwa ni kitendawili.

Akizungumzia kuhusu vibali vya Lwanga Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Barbara  alisema: “Bado tunapambana kuhakikisha tunakamilisha vibali vya kiungo wetu mkabaji, Taddeo Lwanga vinakamilika ili nyota huyo aanze kuitumikia Simba rasmi.

“Tumefikia mahali pazuri katika hilo na ni matumaini yetu kuwa hivi karibuni kila kitu kitakuwa kimekamilika,” .

Nyota huyo alisaini dili la miaka miwili ndani ya Simba akiwa amepewa jezi namba nne ambayo ilikuwa inavaliwa na nyoya, Gerson Fraga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here