Simba SC ushindi lazima leo

0

NA MUSSA KICHEBA

WAKATI Simba SC ikiwa ya moto, uongozi wa timu hiyo, umewataka wachezaji kuongeza kasi kila wanapolikaribia lango la wapinzani ili kujihakikishia kupata ushindi wa mapema katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa, dhidi ya FC Platinum, leo jijini Dar es Salaam.

Ikumbukwe Simba kwa sasa ipo katika presha kubwa ya kushinda mchezo huo ili kufuzu hatua ya makundi, kama ilivyofanya miaka miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Haji Manara, anaamini mchezo utakuwa mgumu lakini anaamini kikosi chake kikijituma kitamaliza kazi mapema.

“Naamini kikosi chetu kitafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa kuitoa FC Platinum ya Zimbabwe katika mchezo wa mkondo wa pili utakaopigwa leo, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam,”alisema Manara.

Manara, alitamba kuwa na uhakika huo, huku akithibitisha kuamini mbinu za kuwa zitasaidia kufikia lengo la kuibuka na ushindi utakaolipa kisasi cha kupoteza mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa mjini Harare, Desemba 23 mwaka jana ambapo Simba SC walifungwa bao 1-0.

Alisema kuwa nafasi bado ipo wazi kwa Simba SC, na bahati nzuri mchezo wa mkondo wa pili kikosi chake kinacheza nyumbani, ambapo pamekua na bahati kubwa ya kupatikana kwa matokeo mazuri.

“Bado tuna nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya makundi licha ya kupoteza mchezo wa kwanza, tunaamini tutapata matokeo mazuri katika mchezo wa leo tukiwa kwenye uwanja wa nyumbani,”alisema Manara.

 

Naye Kocha Mkuu wa FC Platinum ya Zimbabwe, Norman Mapeza, alisema kuwa anatambua uimara wa Simba upo kwenye safu ya kiungo na ushambuliaji, jambo ambalo atahakikisha kuwa wachezaji hao hawawaletei madhara katika mchezo huo wa leo.

 

“Jambo kubwa ambalo tutafanya ni kuongeza nguvu kwenye ulinzi na safu yake ya ushambuliaji,”alisema Mapeza.

Mapeza alikiongoza kikosi chake kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja wa Taifa Zimbabwe kushinda bao 1-0, ana kibarua cha kulinda ushindi huo ili atinge hatua ya makundi huku Simba wakiweka wazi kwamba lazima wapindue meza kibabe kesho Jumatano, Uwanja wa Taifa, Dar.

Mapeza alisema kuwa anatambua uimara wa Simba ulipo kwa kuwa aliwaona walipocheza kwenye mchezo wao wa kwanza, hivyo presha yake ni kwenye viungo.

“Ninawatambua wapinzani wangu, niliwaona kwenye mchezo wetu uliopita na nguvu yao kubwa ipo kwenye viungo hapo ndipo uimara wao ulipo pamoja na safu ya ushambuliaji ambayo ina nguvu.

 “Kwangu mimi naona ni sawa hata nikiwa ugenini nina nafasi ya kupata matokeo, timu kubwa duniani zikiwa ugenini zinashinda na zikiwa nyumbani pia zinapoteza, nimewaambia vijana wangu namna ya kuwazuia na tutashambulia bila kuogopa,”alisema.

Mchezo huo wa leo utachezwa majira ya saa 11:00 jioni, Uwanja wa Benjamin Mkakapa jijini Dar es Salaam.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here