Simanzi Diwani mteule, wajukuu wakiteketea kwa moto

0

NA MWANDISHI WETU,PWANI

DIWANI Mteule wa Kata ya Kikongo wilayani Kibaha Vijijini katika Mkoa wa Pwani Fatma Ngozi pamoja na mjukuu wake mwenye umri wa miezi kati ya saba na nane Ajivin Hamis wamefariki baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana Novemba 9, 2020.

Tukio la kuungua kwa nyumba hiyo na kusababisha vifo hivyo limetokea majira ya saa nane usiku wa kuamkia jana katika eneo hilo ambapo mashuhuda wa tukio hilo walisema kwamba mbali ya kufariki kwa diwani mteule na mjukuu wake watu wengine watano wameokolewa kutoka kwenye nyumba hiyo.

Walisema chanzo cha kuungua kwa nyumba hiyo bado hakijafahamika ingawa baadhi ya mashuhuda walisema huenda ikawa imeungua kutokana na hitilafu ya umeme.Hata hivyo bado haijafahamika kilichosababisha kuungua kwa nyumba hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba uchunguzi zaidi kubaini chanzo cha moto huo ambao umesababisha vifo hivyo ili kubaini ukweli ,hivyo bado wanachunguza na watakapokamilisha uchunguzi watatoa taarifa.

Alisisitiza maiti zimehifadhiwa katika Hospitali Mlandizi wakati wakiendelea na uchunguzi na baada ya hapo watakabidhi kwa ndugu kwa ajili ya shughuli za mazishi.Kwa upande wa majeruhi waliokolewa kwenye nyumba hiyo wanaendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha.§

Hata hivyo aliomba wananchi kutoa ushirikiano na yoyote mwenye taarifa zitakazosaidia kukamilika kwa uchunguzi wa tukio hilo ni vema akaziwasilisha katika jeshi hilo wazifanyie kazi.

Alipoulizwa chanzo cha moto huo amejibu ni mapema mno, wakikamilisha uchunguzi watafahamu kilichosababisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here