Shehena mafuta ya kula kuingizwa sokoni kumaliza uhaba

0

NA MWANDISHI WETU

JUMLA ya tani 48, 200 za mafuta ya kula zinatarajia nkuingia sokoni baada ya kumalizika upakuaji wa shehena ya tani 21,800 huku zingine 26,450 zikiendelea kupakuliwa katika bandari ya Dar es Salaam.

Taarifa ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Godfrey Mwambe jana ilieleza kuwapo kwa upungufu wa mafuta ya kula nchini lakini amebainisha kuwa ni tatizo litakalomalizika mara baada ya kukamilika upakuaji wa shehena ya bidhaa hiyo.

Waziri alisema upungufu huo umetokana na upungufu wa uzalishaji na kutegemea kuyaagiza mafuta hayo kutoka nje hivyo bei yake kubadilika kulingana na mwenendo wa soko la dunia.

Alisema kiasi cha mafuta ya kula yenye ujazo wa 21,800 kimepakuliwa katika meli hiyo na sasa wanaanza kuingiza sokoni.

Waziri alisema meli nyingine ya Melati Satu yenye tani 26,450 za mafuta ilitia nanga Januari 5 na itayashusha kati ya Januari 19 hadiJanuari 22.

Taarifa ya waziri huyo inasema mahitaji ya mafuta nchini ni tani 570,000 kwa mwaka lakini uzalishaji uliopo ni tani 205,000.

“Serikali imezipa leseni kampuni mbili kuagiza mafuta ya kula ambazo ni East Coast Oil and Fats na Murzah Wilmar East Africa, kampuni hizo zitaingiza mafuta ya kula nchini ili kukabili upungufu wa tani 365,000,” alisema Mwambe.

Waziri alisema meli ya UACC Shimiya iliwasili bandarini tangu Desemba 10 mwaka jana na ilipangwa kushusha shehena Januari 11 lakini iliruhusiwa kuanza kushusha shehena Desemba 30 na kukamilisha ushushaji Januari 03.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here