SHANGWE BAGAMOYO

0

NA HAFIDH KIDO, BAGAMOYO

HADHI ya Mji mkongwe wa Bagamoyo mkoani Pwani inakwenda kurudishwa kutokana na ahadi iliyotolewa jana na mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni za chama hicho katika viwanja vya Mwanakalenga wilayani humo jana, Dk. Magufuli alisema mji huo mkongwe hauna budi kuenziwa kwa sababu mbali ya kuzaliwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete lakini pia wakati wa ukoloni yalikuwa makao makuu ya nchi kabla ya kuhamishiwa Dar es Salaam na baadaye Dodoma.

“Bagamoyo lazima turudishe heshima zake. Ilijulikana tangu enzi na enzi. Hapa ndio ilikuwa makao makuu ya nchi lazima mioyo ibwagwe hapa,” alisema na kusisitiza:

“Endapo mtatuchagua  tena lengo  letu kuu  ni kuhakikisha  utalii wa kihistoria  na  malikale  unafanyika  Bagamoyo  ambao  ni mji wenye  historia kubwa, vilevile nataka  pale Chalinze iwe wilaya, ninaomba  mniletee wabunge na madiwani ili waweze  kukaa  pamoja  na kupanga maendeleo  ya  Wilaya ya Chalinze.”

Alisema, amepita Mkoa wa Pwani kuwaomba kura wananchi kwa sababu katika miak mitano iliyopita Serikali ya Awamu ya Tano iliyoongozwa na CCM ilifanya mambo makubwa ya kimaendeleo katika mkoa huo ikiwemo katika sekta za afya, maji, elimu na miundombinu ya barabara.

“Tumejenga shule, madarasa, maabara na kukarabat shule kongwe tano ikiwemo Ruvu, Kibaha, Minaki, Kibaha na Kibiti. Vilevile tumejenga shule ya ufundi Wilaya ya Rufiji Kata ya Chemchem. Kwa sababu hatutaki motto wa maskini akose elimu kwa kukosa fedha.

“Vilevile tumejenga hospitali za Wilaya sita katika Wilaya za Mafia, Kibiti, Kisarawe, Mkuranga, Kibaha na Chalinze.

Vituo vya afya 18, tumeleta magari ya wagonjwa 12 hivyo kufanya mkoa huu kuwa na magari ya wagonjwa 36 pamoja na kuajiri watumishi wa afya 896,” alisema na kuongeza:

“Miaka mitano ijayo tutaendeleza ujenzi wa miundombinu ya afya ikiwemo hospitali, vituo vya afya na zahanati. Tunataka Watanzania wote wawe na huduma nzuri za afya.”

Katika maelezo yake mgombea huyo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Watanzania alisema katika mkoa huo kumetekelezwa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya Sh Bilioni 185.4, mradi mwingine wa Ruvu Juu wenye thamani ya Sh Bil 105.8. Vilevile kuna mradi wa maji ya visima kutoka Mtera na Rufiji.

Kuhusu miundombinu ya usafirishaji mbali ya mradi wa reli ya kisasa (SGR) uliofikia asilimia 95 kukamilika, utasaidia kukamilishwa kwa bandari kavu ya Kwale upo pia mradi wa  Daraja la Wami lenye urefu wa mita 513 kwa thamani ya Sh Bil 67.8.

Kuna miradi iliyokamilika ya barabara ya Bagamoyo hadi Msata ulioondoa adha ya usafiri katika mkoa huo, pia kuna miradi ya barabara za mjini zenye jumla ya kilomita 11 ikiwemo kilomita mbili zilizopo Bagamoyo.

“Barabara nyingine zinakamilishwa kutoka Kisarawe hadi Mwaneromango, Makurunge – Saadani hadi Tanga yenye urefu wa kilomita 178 itakamilishwa na fedha zipo ili Mzee Kikwete akitaka kwenda Tanga achague anatumia njia ya Chalinze au ya pembezoni mwa bahari.

“Ipo pia barabara ya kutoka Makofia hadi Vikurumbu yenye urefu wa kilomita 148, barabara ya Kibaha – Mapinga (km 23) na Utete – Nyamwage yenye urefu wa kilomita 33.7 zote kwa kiwango cha lami na fedha zipo,” alisisitiza Dk. Magufuli.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli alizungumzia kero sugu yamuda mrefu juu ya migogoro ya wananchi na hifadhi za taifa pamoja na mapori tengefu, alisema uamuzi ulifanyika na utaendelea kufanyika kurasimisha maeneo ili yamilikiwe na wanavijiji.

“Kero kubwa ya migogoro hifadhi, ranchi za taifa na wawekezaji tunajitahidi kuzitatua hasa baada ya kurasimisha vijiji 89 vilivyokuwa sehemu ya hifadhi,” alisema na kuvitaja baadhi ya vijiji hivyo kuwa ni pamoja na:

“Kitonga, Milo, Mkenge, Kidomole, Fukayosi, Kaole Ufundi, Kihalaka, Mwaluhongo, Pongwe, Msukura, Kisungura, Vigwaza, Chamalweza, Kwa Zoka, Ruvu Darajani, Mwidu, Tukamisasa, Mindu, Kizangu, Niazile, Kitame, Matipwiri na Saadani ambapo vitongoji vitaondolewa katika umiliki wa hifadhi kuwa makazi ya wananchi.”

Akizungumzia suala la viwanda, Dk. Magufuli aliwapongeza wananchi wa Pwani kwa kuona fursa kwenye uwekezaji ambapo mkoa huo ndio unaoongoza kwa idadi kubwa ya viwanda kuliko mikoa yote Tanzania.

“Mkoa wa Pwani  hongereni sana, mwaka  2015 kulikuwa  na viwanda 395, sasa kuna viwanda  1,236 ni hatua kubwa sana na mkoa  huu ndio unaoongoza  kwa viwanda Tanzania  nzima.

“Tumempatia  Bakhresa  ekari 10,000 za ardhi  kwa  ajili ya  kuanzisha shamba  la miwa mwakani, shamba  hilo  linatarajia  kuzalisha  sukari  tani  30,000 hadi 35,000 huku  watu 800 wakitarajiwa kuajiriwa na baadaye zaidi  kuzalisha tani  60,000 hadi  70,000 na kuzalisha  zaidi ya ajira 2000, wana Pwani  hii ni fursa kubwa  ya ajira kwenu,” alisema Dk. Magufuli.

Katika uwekezaji mkubwa wa uchumi wa bluu (Blue Economy) Dk. Magufuli alisema atahakikisha wavuvi wadogo na wakubwa wanatumia vizuri fursa ya bahari iliyopo mkoani humo kunufaika.

“Tunataka  kuwe na sheria ya usimamizi wa uvuvi  wa bahari ili wawekezaji  wawekeze katika  uvuvi  na  kuwa  na viwanda  vya uchakataji  wa samaki vitakavyotoa ajira na upatikanaji  wa uhakika  wa kitoweo,” alisema na kuongeza:

“Tumeokoa zaidi ya Sh Bil 118 kutoka shirika la uvuvi (TAFICO), tumejipanga tutanunua meli nane ambazo nne zitakuwa upande wa Tanzania Bara na nne za Viziwani Zanzibar ili tufanye uvuvi wa kisasa, ndiyo maana tulifuta tozo tano za uvuvi na tutaendelea kuzipitia kero za wavuvi ili tuwapunguzie kero zinazowarudisha nyuma kupata maendeleo kwenye shughuli zao.”

Alieleza pia juu ya utalii wa baharini ambapo aliwaeleza wananchi wa Bagamoyo kuwa kutakuwepo na meli ya kitalii itakayowazungusha wageni pamoja na kuimarisha miundombinu  ya kimkakati kuwezesha wataluii kuja kwa wingi kuangalia maeneo ya kihistoria na mali kale.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo aliwakumbusha wananchi wa Pwani kuwa kazi iliyobakia katika miaka mitano ijayo ni kuimarisha masuala ya afya, maji, miundombinu na umeme na usafiri.

Alieleza pia mkakati wa kuvimalizia vijiji vyote 2,500 vilivyobakia bila umeme nchi nzima hasa kutokana na kuwepo mradi mkuba wa kufua umeme wa Julius Nyerere utakaozalisha Megawati 2115 za umeme.

Kuhusu wafanyakazi Dk. Magufuli alisema atahakikisha anaongeza maslahi ya wafanyakazi katika miaka mitano ijayo kwa kuwa tayari mikakati ya kukuza uchumi kwa kutumia rasilimali za ndani imefikia malengo.

“Tumepanga kuongeza maslahi ya wafanyakazi. Kwa sababu uchumi tumeshaujenga na mapato yanapatikana, tumepanga kuwaongezea mishahara na marupurupu yao wafanyakazi,” alisema Dk. Magufuli.

Aliwakumbusha pia wananchi kujali amani na utulivu wa nchi hasa kwa kipindi hiki cha uchaguzi ambapo baadhi ya wanasiasa wanaeneza maneno ya chuki, alibainisha wanasiasa hao wasipewe nafasi na ikibidi wafundishwe adabu kwa kunyimwa kura.

“Amani ni  lazima tuilinde kwelikweli, msiwasikilize watu wanaohubiri vurugu, Tanzania  tunahitaji  amani  na tukumbuke  kuwa  kuna  maisha  baada  ya uchaguzi, huu  ni uchaguzi  kama  chaguzi  nyingine ni  lazima  tudumishe amani na tuilinde kwa nguvu  zetu  ili tuendelee kuijenga  nchi yetu baada ya uchaguzi,” alisema Dk.  Magufuli na kusisitiza:

“Uchaguzi huu ni kati ya kuchagua vibaraka wa mabeberu au walinda nchi, wavuruga amani au walinzi wa amani au wanaotuletea ubaguzi wa ukanda na ukabila au wanaotuleta pamoja.

“Kuchagua watu wanaotaka kuturudisha katika utegemezi wa misaada au kujitegemea. Wanaolinda rasilimali au kuweka rehani rasilimali zetu kwa watu kutoka nje. Kuchagua watu wenye jitihada ya kujenga miundombinu au wanaotaka tusiendelee kujenga miundombinu. Viongozi watakaolinda desturi na tamaduni zetu au wanaotaka kutuletea desturi za kigeni ambazo ni mpya zisizokubalika.”

Awali, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alimzungumzia Dk. Magufuli kama kiongozi wa kipekee aliyeleta mabadiliko makubwa Tanzania.

“Kazi ya kampeni naijua vema ni ngumu na inachosha, lakini inaleta faraja unapoona kuna watu wanakusubiri kwa wingi wakiwa na sura za bashasha roho inakua baridiii. Pole na hongera sana ndugu rais na mgombea kwa kazi kubwa uliyoifanya, sina wasiwasi tutashinda kwa kishindo.

“Hatuna sababu ya kushindwa katika urais, ubunge na udiwani kwa sababu kazi kubwa uliyoifanya kwa miaka mitano inaonekana, CCM katika mikono yako imefanya mambo makubwa shukurani yao ni kukupigia kura tarehe 28. Tanzania ya leo si ile niliyoiacha maka 2015, tunataka nini tena,” alihoji Kikwete.

Rais Magufuli akisalimiana na Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete akiwa njiani Msata Bagamoyo Mkoani Pwani wakati akielekea Mkoa wa Tanga.

Hadi jana zilikuwa zimebakia siku tisa kabla ya kupiga kura Oktoba 28, 2020  ambapo Dk. Magufuli anaendelea na kampeni zake katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara kabla ya kuwasili Dodoma kwa ajili ya kupiga kura.

Leo atakua na mkutano mkubwa katika Wilaya ya Korogwe ambapo utawakilisha Mkoa wa Tanga kwa ujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here