Serikali kuendelea kusimamia maadili katika utumishi wa Umma, kupambana na rushwa

0

NA DOTTO KWILASA,DODOMA

KATIKA kuadhimisha siku ya maadili na haki za binadamu, utekelezwaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi umekuwa ukidumazwa kwa kiasi kikubwa na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ambako kunachangiwa na ukosefu wa maadili miongoni mwa baadhi ya watendaji serikalini na sekta binafsi.

Kufuatia kuwepo kwa changamoto hiyo ,Serikali imesema itaendelea kusimamia maadili katika utumishi wa Umma ,kupambana na vitendo vya rushwa na kusimamia haki za binadamu .

Hayo yamebainishwa jijini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) George Mkuchika wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu.

Mkuchika alisema kupitia taasisi na vyombo vilivyopewa majukumu ya kusimamia maadili itazidi kuongeza ufanisi wake katika kusimamia misingi ya maadili na utawala bora ili kuwa na Tanzania yenye amani.

Licha ya hayo aliongeza kuwa Juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na utawala bora zinatambulika ndani nan je ya nchi ambapo katika miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa ikitolewa mfano wa nchi zilizofanikiwa katika masuala yay a uadilifu ,mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mazuri ya rasilimali za nchi kuwaletea wananchi maendeleo.

“Tumejipanga kukumbushana umuhimu wa kuzingatia misingi ya ahadi ya uadilifu ambayo ndiyo mwongozo wa mwenendo wa watumishi waliopewa dhamana ya kuwahudumuia wananchi ,watumishi wa sekta ya umma pamoja na wale sekta binafsi tunao wajibu wa kuzingatia misingi ya ahadi hiyo,”amesema .

Aidha kwa kutambua changamoto za rushwa na ukosefu wa maadili kwa baadhi ya taasisi, serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa na Mpango wa utekelezaji awamu ya tatu ambao ulizinduliwa Desemba 10,2016.

“Mkakati huu unaainisha majukumu ya kila sekta hivyo wadau wote wanapaswa kuupitia na kuhakikisha wanatoa mchango kwa jamii katika mapambano dhidi ya rushwa nchini kwani ni jukumu la kila mtanzania,” alisistiza.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here