Serikali ilivyofanikiwa kudhibiti bei ya saruji

0

NA WAANDISHI WETU

NI ngumu sana kuamini kuwa kelele za tatizo la upatikanaji wa saruji na kupanda kwa bei zingezimika kabla hata mwaka haujaisha.        Ni wiki mbili tu tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akutane na Wadau wa bidhaa hiyo kujadili na kufikia mwafaka wa kumaliza tatizo hilo, na sasa hakuna tena kelele za uhaba wala bei kubwa ya saruji.

Ukimya huo unamaanisha kwamba kikao cha Waziri Mkuu na wadau, kimezaa matunda ndani ya muda mfupi  licha ya kwamba bado bei hazijashuka hadi kiwango kinachotakiwa lakini imeshuka kwa kiasi kikubwa.

Wakati wiki mbili zilizopita bei ya mfuko mmoja wa saruji Jiji Dar es Salaam ulikuwa Sh 15,000, hadi jana mfuko huo ulikuwa Sh 14,000 lakini waziri Mkuu aliagiza kwa Dar es Salaam unatakiwa kufikia Sh 12,700 hadi 13,800.

Haya ni matokeo ya kazi kubwa aliyofanya Waziri Mkuu Majaliwa kwanza kwa kutaka kujua kiini cha tatizo ambapo baada ya majadiliano ilionekana hakukuwa na sababu za msingi za kupanda kwa bei na kuadimika kwa saruji nchini.

Waziri Mkuu alisema bei ya viuwandani ilikuwa hajabadilika licha ya kuwepo malalamiko ya baadhi ya mawakala kucheleweshewa mzigo hivyo kusababisha uhaba ambao ulisababisha mawakala wenye tamaa kutumia tatizo hilo kama fursa ya kuongeza bei ya bidhaa hiyo.

Katika kikao hicho ilibainika kuwa hakuna gharama hata moja iliyoongezeka katika mnyororro wa uzalishaji wa saruji bali kuadimika kwake ndiko kulikosababisha watu kupandisha bei ili kupata faida kubwa kutokana na mahitaji kuwa makubwa. Hata hivyo waziri mkuu aliagiza viwanda vinavyozalisha saruji kuweka utaratibu mzuri wa kugawa saruji kwa mawakala bila kuchelewa na kuagiza mamlaka zinazohusika kutembelea viwanda hivyo.

Hii inaonyesha kuwa hata viwanda vilikuwa havina sababu ya kuchelewesha mzigo na ndiyo maana sasa hatusikii tena habari za bei kubwa ya saruji au uhaba.

Mfano mwingine ni mkoani Tanga ambako tunaelezwa kuwa bei ya saruji kwa mfuko mmoja imefikia Sh 13,500 kwa rejareja.

Waziri Mkuu alionyesha wazi kuwa kuna namna fulani ya kuhujmiwa kwa Serikali hasa kutokana na kuwa ni kipindi cha uchaguzi ili kuichonganisha Serikali na wananchi wake.

“Kumekuwa na tabia ya bei za saruji kupanda wakati wa Uchaguzi na hizi ni kampeni za hovyo zinazofanywa na watu wachache ili kuweka migogoro kati ya Serikali na wananchi. lakini pia ni kuwafanya wananchi kutokuwa na imani na Serikali iliyoko madarakani,” alisema Majaliwa.

Wapo waliosingiza tatizo la miundombinu kama vile umeme lakini Waziri Mkuu alisimama kidete na kueleza namna Serikali ilivyowekeza katika uzalishaji wa umeme na kwamba kama ni tatizo la umeme haliwezi kudumu kiasi cha kuathiri uzalishaji.

“Kuna habari zilikuwapo kwamba Viwanda vya Tanga vilikosa umeme, lakini RC alipoenda akakuta sio taarifa rasmi na niwaambie nchi hii katika umeme tumefanya vizuri sana na ikitokea umeme hakuna basi ni tatizo tu katika Kituo cha eneo husika na tatizo huwa sio la muda mrefu.

“Naposema miundombinu iko safi basi wote ni mashahidi kwamba barabara zetu nyingi ambazo ndiko mawakala wanakopita ni za lami, ni maeneo machache ambako kuna barabara za vumbi na tutapeleka lami siku siyo nyingi, hivyo mawakala wanaosambaza saruji hawana tatizo la kukumbana na barabara mbovu,” alisema Majaliwa.

Majaliwa aliwaonya Mawakala wanaopandisha bei na kueleza kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuhujumu uchumi wa Taifa.

“Mawakala mnapoweka bei kubwa Ili bidhaa ziwe ngumu kupatikana kwa wananchi huo ni uhujumu uchumi na tukitumia Sheria namba 200 ya 2019 ya uhujumu uchumi basi mtashitakiwa, tukija kukagua na tukakuta mna bidhaa wakati mtaani hazipo utakamatwa kwa kosa la uhujumu uchumi,” alisema Majaliwa.

Kikao hicho kiliishia kwa kutoa maagizo kwa taasisi mbalimba za Serikali ambayo bila shaka yanaendelea kufanyiwa kazi na ndiyo msingi wa utulivu tunaoushuhudia hivi sasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here