Samatta azua hofu, kocha asema timu itafanya vizuri

0

NA SHEHE SEMTAWA

KIKOSI cha Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kikiwa tayari kuivaa Tunisia kesho kusaka tiketi ya kushiriki AFCON, Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta ataikosa mechi hiyo na mechi ya marudiano kutokana na kuumia akiwa na klabu yake ya Fenerbahce.

Kukosekana kwa nahodha huyo wa Stars kumepokelewa kwa mshtuko mkubwa na baadhi ya wadau huku wakitoa maoni mbalimbali kuelekea mchezo huo.

Ikumbukwe KIKOSI cha Taifa Stars tayari kipo Tunisia baada ya kambi ya siku tatu Jijini Istanbul nchini Uturuki kujianda na mchezo wa Kundi ‘J’ dhidi ya wenyeji wao hao, kufuzu AFCON ya 2021 Cameroon.

Mechi itachezwa kesho Ijumaa Uwanja wa Hamadi Agrebi Olimpiki mjini Rades, kabla ya timu hizo kurudiana Dar es Salaam siku nne baadaye na mechi zote zitaonyeshwa LIVE na chaneli ya ZBC 2 inayopatikana katika kisumbusi cha Azam TV.

Akizungumzia kama kuna athari yeyote ya kukosekana Samatta, Kocha wa mpira wa miguu, Moses Wiliam, alisema “Ni hasara kubwa kukosekana ubora wa Popa kama Nahodha wa kikosi cha timu yetu ya Taifa.

“Lakini pia uwelewa wa kimbinu kwake umekomaa ni kwa sababu kacheza vilabu tofauti tofauti, kakutana na walimu tofauti tofauti wenye mifumo tofauti, tofauti.

“Kwa hiyo kipo kipindi ambacho alishambulia kutokea pembeni ambacho alikuwa anacheza kama mshambuliaji wa pili, kuna kipindi alikuwa nacheza kama mshambuliaji pacha.

“Kuna kipindi alisimama pekeake kwa hiyo ameshakuwa ana badilishwa badilishwa kutokana na aina ya mwalimu na mfumbo ambao unatumika.

“Kwa hiyo kumkosa mchezaji wa aina hii, kwa rasilimali watu tulizo nazo za wachezaji Tanzania ni bonge moja la pengo lakini kwa upande mwingine naona ni fursa ya wachezaji wengine kufurahia mpira.

“Kwa sababu kuna namna Fulani ambayo akiwepo Popa hata kama watu watakataa, labda kina Sure Boy kina Mkude ni lazima mpira wake wakwanza tu anajaribu kumuangalia Popa amekaaje labda kama amebanwa, chaguo la pili ndio atamuangalia mtu mwingine,”.

Naye Lawena Nsonda, aliwashauri Watanzania kuwa wasikate tamaa kwa kukosekana Samatta katika mchezo huo dhidi ya Tunisia huku akiamini matokeo yatakuwa mazuri zaidi.

“Inawezekana timu inafanya vibaya kwa sababu wachezaji wanajua kwamba kuna mchezaji ambaye ni bora, we mwenyewe ni shahidi tumecheza na timu ya Burundi juzi hapa tulishindwa kabisa kucheza tukafungwa goli moja.

“Kwa hiyo vijana kwa sababu watajijua tumebaki sisi kama sisi watacheza vizuri kabisa na watajituma na lazima tunaweza tukapata ushindi, kwa hiyo ningependa kuwaambia Watanzania wasikate tama kwa kukosekana Samatta nadhani mambo yatakuwa mzuri zaidi.

Kocha Mkuu wa Stars, Ettiene Ndayiragije alisema kuwa wachezaji wapo vizuri ila watakosa huduma ya Samatta ambaye anapaswa kupumzika kwa muda wa wiki mbili.

“Wengine wapo ambao watacheza nafasi yake na itakuwa ni faraja kwake kuona tukipata ushindi,” amesema.

Wakati huo huo shiriksho la soka barani Afrika CAF, limetangaza orodha ya waamuzi watakaochezesha mchezo wa mzunguuko wa tatu wa kundi J kati ya Tanzania na Tunisia utakaochezwa Ijumaa Novemba 13 mjini Tunis.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here