RC Wagambo apigilia msumari wa mwisho miradi ya shule ya Bil 1.15/-

0

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia miradi yake ya Afya na Usafi wa Mazingira (SWASH) Pamoja
na mradi wa Lipa kulingana na Matokeo (EP4R) imeipatia Halmashauri ya
Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa jumla ya Shilingi 1,152,557,008.77/=
kutekeleza ujenzi wa madarasa 18, matundu ya vyoo 178 na mabweni mawili.

Miradi hiyo itatekelezwa katika Shule za Msingi na Sekondari, fedha ambayo
halmashauri hiyo ilipatiwa tangu Juni, 2020 lakini hadi kufikia Disemba 2020
ujenzi haujafikia hata asilimia 50.

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amekemea
uzembe unaofanywa na viongozi wa halmashauri hiyo huku akisikitishwa na
kitendo cha Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo Msongela Palela kuchukua ruhusa
ya kuondoka nje ya mkoa huo huku katika halmashauri yake kukikosekana
madarasa saba kwa ajili ya wanafunzi 254.

Aidha, mbali na fedha za miradi hiyo wananchi wa Kata ya Matai kwa kushirikiana na halmshauri wameanza ujenzi wa vyumba vya madarasa manne katika Shule ya Sekondari Matai ambavyo vinatakiwa kukamilika kabla ya Februari 28 mwakani kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza ya uchaguzi wa wanafunzi hao wilayani humo.

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya shule za Msingi za Sekondari katika Halmshauri hiyo, akiwa katika Shule ya Sekondari Matai, Wangabo alisema amekosa imani na utendaji kazi wa halmashauri hiyo baada ya kuona miradi inayogharamiwa na serikali kutomalizika kwa wakati.

“Miezi sita lakini watu wanafanya utekelezaji kwa asilimia 42, sasa mimi inanipa mashaka, huku tu ambako kuna fedha ujenzi haujakamilika kwa miezi sita, je huku ambako tunaanza msingi na hakuna fedha ni juhudi za wananchi; tutakamilisha baada ya muda gani?,” alihoji.

Aidha, Aliutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kufanya kazi ya ziada ili kutekeleza maagizo ya serikali ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanaendelea na masomo yao kama ilivyoelekezwa.

Wakati akitoa taarifa ya Wilaya hiyo Mkuu wa Wilaya hiyo, Carolius Misungwi alieleza mikakati mbalimbali iliyowekwa na Wilaya ili kufanikisha azma ya serikali katika kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa madarasa hayo na wanafunzi hao kuendelea na masomo ifikapo Februari, 2021.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here