RC Tabora awataka madiwani kudhibiti matumizi ya fedha za ummaa

0
Baadhi ya Madiwani wa Manispaa ya Tabora wakiwa katika kikao chao cha kwanza cha Baraza jana.

NA TIGANYA VINCENT, RS TABORA

MKUU wa Mkoa wa Tabora Dk.Philemon Sengati amewataka Madiwani kusimamia na kudhibiti matumizi ya fedha za umma ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuwasaidia ya kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Alisema fedha zote ni lazima zitumike kwa kuzingatia mipango na bajeti za Halmashauri na Serikali kwa ujumla kupitia Sheria ya Bajeti na ile ya fedha za umma.

Dk. Sengati alitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa Baraza jipa ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.

Alisema Madiwani wanalojukumu la kuhakikisha kuwa fedha zote zinazoletwa na Serikali kuu na zile walizokusanya zinatumika kwa usahihi na uwazi na kuzipeleka katika shughuli mbalimbali za wananchi.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema hatua hiyo itasaidia kuepuka matumizi yasiliyokuwemo katika bajeti waliyopitisha ambayo yanarudisha nyuma maendeleo na kuwasonesha wananchi.

Dkt. Sengati alisema ili kudhibiti ufujaji wa makusanyo ya Halmashauri ni lazima fedha zote zikusanywe kwa kutumia mashine(pos) na kutoa stakabadhi kwa waliotoa fedha.

Alisema ni marufuku kwa watendaji waliopewa dhamana ya kukusanya mapato kutumia vitabu kuandika kwa mkono wakati wa makusanyo ya mapato ya Halmashauri kwa kuwa njia hiyo ndio inayotumika kuiba fedha za umma kwa kutoa taarifa zisizoshaihi za ukusanyaji wa fedha.

Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa Madiwani wanalo jukumu la kuhakikisha kuwa hakuna fedha inayotumika kabla ya kupelekwa benki.

Alisema utumiaji wa fedha ambazo hazipita Benki(fedha mbichi) unasababisha kuzalishwa kwa hoja za kiugazi na wakati watendaji wasio waadilifu kutumia nafasi hiyo kuiba fedha za umma.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Madiwani kuhakikisha wanasimamia na kuwahimiza watendaji katika maeneo yao kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuiwezesha Manispaa ya Tabora kuwa na fedha nyingi zitakasaidia katika shughuli za maendeleo ya wananchi.

Alisema ni lazima wajipange kuhakiksha kuwa ifikapo mwaka 2025 wanakuwa na mapato ambayo watakuwa tena hawategemei fedha za ruzuku kutoka Serikali kuu.

Katika hatua nyingine Madiwani wa Manispaa ya Tabora wamemchagua Diwani wa Kata ya Isevya Ramadhan Kapera kuwa Mstahiki Meya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here