Rais Magufuli kuhutubia Bunge kesho

0

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

RAIS Dk. John Magufuli anatarajiwa kulihutubia Bunge la 12 kesho Ijumaa Novemba 13, 2020,  saa 3:00 asubuhi, Dodoma,  kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Bunge.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma mapema jana  Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema desturi ya Bunge linapoanza mara baada ya kutoka katika uchaguzi kuna hotuba ya rais wa nchi kuhutubia Watanzania.

Alisema hotuba hiyo ya Rais ni muhimu sana kwani ndiyo inatoa dira ya Serikali kwa miaka mingine mitano.

“Ninawataka Ijumaa saa tatu kamili asubuhi kuhudhuria tukio hilo bila kukosa kumsikiliza mheshimiwa rais atakachosema. Waheshimiwa wabunge najua mmewasili kwenye siku kadhaa sasa lakini baada ya kuapa tu hapa, sasa mambo yote tutarekebisha yanayohusiana na utaratibu. Pia natambua kuwa waheshimiwa wabunge mnao wageni wengi, mnayo mambo mengi ya kurekebisha hapa mjini.

“Wengine bado mambo ya makazi hayajakaa sawasawa, wengine simu za wajumbe bado nyingi sana…… Wajumbe bado wanafatilia, lazima upate muda wa kuwasiliana na wajumbe. Wabunge ni watu wenye shughuli nyingi sana kwa hiyo tumeona mchana wa leo tuwaachie muwe huru mrekebishe mambo yenu ili tuweze kukutana kesho saa tatu kwa shughuli za kesho kwa maana hiyo naahirisha shughuli za bunge mpaka kesho saa tatu,” alisema Ndugai.

Rais alizungumza nini ufunguzi wa Bunge lililopita?

Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la 11 ambalo ilikuwa mara yake ya kwanza Rais Magufuli alitumia muda mwingi kueleza kwa kina kile ambacho angekifanya katika miaka mitano ya awamu yake ya kwanza.

Aliorodhesha kero kubwa za wananchi alizokutana nazo wakati wa kampeni na kutoa mwelekeo wa namna ya kuzitatua katika kipindi chake.

Miongoni mwa mambo ambayo aliyaorodhesha ni pamoja na kuwepo kwa rushwa, ufisadi, uzembe na matumizi mabaya ya fedha za umma. Pia alitaja wizi wa madini, wizi wa mizigo na ucheleweshaji wa huduma bandarini, upitishaji wa madawa ya kulevya mipakani pamoja na utoroshaji wa madini.

Alitaja uwepo wa kero katika huduma za jamii kama hospitali, shule na huduma za maji na miundombinu ya barabara. Haya ni baadhi ya mambo aliyoyagusa na kuahidi kuyafanyia kazi katika miaka mitano.

Kwa kiasi kikubwa Rais Magufuli alitekeleza ahadi zake kwa miaka mitano na mwisho wa Bunge alikwenda kulifunga na kueleza namna alivyotekeleza yale yote aliyoahidi.

Ni kiu ya kila Mtanzania kutaka kujua kile hasa ambacho Rais Magufuli atakwenda kueleza katika ufunguzi wa Bunge la 12 ikiwa ni bunge lake la mwisho kufikia 2025 mwaka ambao Tanzania inafikia ukomo wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa miaka 25.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here