Rais Magufuli azindua msikiti wa Aboubakary bin Zubeir Chamwino

0

NA HAFIDH KIDO, DODOMA

RAIS Dk. John Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na kuvumiliana katika dini kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa msikiti huo uliopewa jina la Masjid Mufti Aboubakar bin Zubeir karibu na ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya mchango wa waumini wa dini zote nchini, alisema hiyo ni ishara njema ya mshikamano wa kidini.

Aidha, msikiti huo uliojengwa kwa mwesi mmoja na siku 28 umegharimu jumla ya Sh Bilioni 319.3 fedha zake zilianza kuchangwa wakati Dk. Magufuli akiwa katika uzinduzi wa Kanisa la Katoliki Maria Ikulata lililopo Chamwino jijini humo baada ya kuonekana haja ya kuwa na msikiti karibu na eneo hilo la ikulu.

“Kitabu cha Qurani kinasema anayeshiriki ujenzi wa msikiti Mwenyezi Mungu atamjengea mji mbinguni. Msikiti ni nyumba ya kulitaja na kulinyanyua jina la Mungu, ndiyo maana tulianza uchangiaji ambapo watu wa dini mbalimbali, wafanyabiashara na viongozo wa chama changu cha CCM walichangia.

“Nilipouona wakati wa ujenzi nikasema kuwekwe na ofisi ya Mufti na nyumba ya kulala Mufti ili Sheikh Aboubakar Zubeir asiwe na sababu ya kusema hawezi kuja Dodoma kwa sababu hana pa kulala,” alisema Dk. Magufuli.

Alibainisha Mufti Zubeir ni kiongozi wa kipekee anayependa amani, mshikamano na kukataa udini, hivyo anaona amewaenzi waasisi wa taifa hili kwa vitendo.

“Msikiti huu utukumbushe kuwa tuna wajibu wa kumtanguliza Mungu katika maisha yetu yote,” alisema Dk. Magufuli na kusisitiza kuwa kuwepo na michango kutoka watu wa imani tofauti, makabila na rangi tofauti ni ishara njema kuwa Watanzania wapo pamoja.

Katika hatua nyingine, baada ya Dk. Magufuli kuelezwa kuna kiasi cha fedha kimebaki katika ujenzi huo, aliamrisha fedha hizo kiasi cha Sh Mil 1.1 kiingizwe katika mchango mpya wa ujenzi wa Kanisa la Wasabato.

“Nataka siku moja hapa Chamwino kila madhehebu wawe na nyumba ya ibada. Nataka hii ikulu izungukwe na misikiti na makanisa. Hivyo tayari tumeshajenga kanisa la wanaosali Jumapili, tumejenga msikiti kwa wanaosali Ijumaa na sasa bado kanisa la wanaosali Jumamosi,” alisema Dk. Magufuli.

Awali, Mufti Bin Zubeir wakati akitoa neno la shukurani alisema kujengwa kwa msikiti huo kwa nguvu za Dk. Magufuli amewafanyia waislamu ukarimu mkubwa katika uongozi wake.

“Hatushangai kwa msikiti huu tu kwani tayari ulishatuombea msikiti mkubwa wa kimataifa uliojengwa Kinondini jijini Dar es Salaam uliojengwa na Mfalme wa 16 wa Morocco. Umefanya haya kwa kuwa kila unachokifanya unamtanguliza Mungu mbele,” alisema Mufti Bin Zubeir.

Aidha alifafanua kuwa wapo baadhi ya Waislamu watajiuliza inakuwaje watu wasio waislamu wanachangia ujenzi wa msikiti kuwa ni kutokana na kuwa na elimu ndogo ya dini.

“Elimu ndogo ndio udhia, kwa sababu Mtume Muhammad alishapokea zawadi kutoka kwa wasio waislamu. Waislamu tunazipokea heri hizi. Vilevile kuna zaidi ya haya ulitufanyia kwa kurudisha mali za Waislamu zilizopotea,” alisema Mufti Bin Zubeir.

Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakary bin Zubery

Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Charles Mbuge alisema ujenzi wa msikiti huo ulianza Agosti 28, 2020 baada ya kupewa agizo la kuanza ujenzi kutoka kwa Rais Dk. Magufuli mnamo Agosti 25 mwaka huu.

“Fedha zilizokusanywa ilikuwa jumla ya Sh Mil 319.2 ambapo laiti ujenzi huu usingesimamiwa na JKT ungegharimu Sh Mil 439.4. Fedha zilizobaki baada ya ujenzi kukamilika ni Sh Mil 1.1.

“Baada ya kukamilika msikiti huu utaingiza waumini 500 ambapo awali walikuwa wakiingia waumini chini ya 150. Vilevile kuna ofisi ya Mufti,” alisema Meja Jenerali Mbuge.

Fedha za ujenzi huo zilianza kukusanywa katika Kanisa Katoliki Maria Emakulata ambapo zilipatikana jumla ya Sh Mil 25.6, baadaye Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wafanyabiashara, waumini, wakuu wa mikoa na wilaya walichangia hadi zikafikia Sh Mil 319.2.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here