Rais Magufuli atoboa siri ya kumteua Profesa Manya

0
Rais Dk. John Magufuli akimuapisha Profesa Shukrani Manya kuwa Naibu Waziri wa Madini katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma leo Disemba 11, 2020.

Na Mwandishi Wetu 

Rais Dk. John Magufuli ameeleza siri ya kumteua Profesa Shukrani Manya kuwa naibu waziri wa madini baada ya aliyemteua awali, Francis Ndulane kushindwa kula kiapo juzi Desemba 9, 2020.

 Akizungumza leo Ijumaa Desemba 11, 2020 baada ya kumuapisha Profesa Manya ambaye amemteua leo kuwa mbunge, Rais Magufuli amesema wamemchagua yeye kwa sababu ya taaluma yake ya madini ili akawe kiungo katika wizara hiyo.

“Tumekuchagua wewe kwa sababu tuliona wizara hii kwenye nafasi za juu inayumba professionally kwa sababu waziri hajui madini, yeye profession yake ni mwalimu. Katibu Mkuu yeye ni profesa lakini amechukua mambo ya computer au statistics…,tumeona tukuweke wewe ili ukawe link nzuri kwenye wizara hii,” amesema Rais Magufuli.

Amesema licha ya kwamba yeye ni Profesa, haimaanishi kwamba maprofesa wote waliowahi kukaa katika wizara ya madini walifanya vizuri, “tumewahi kuwa na waziri profesa, tumewahi kuwa na katibu mkuu profesa, tena wa madini. Mambo hayakuenda vizuri…, usije ukaangukia kwenye mtego huo.”

Amesema, “Tanzania ina madini ya kila aina, kuna madini ya chuma, kwa nini chuma hakitumiki kutengeneza nondo badala yake vyuma vya reli ndiyo vinatumika. Sekta ya madini ni sekta muhimu, mkijipanga vizuri mkahusisha wataalamu vizuri, mkashirikiana kweli kweli mkiamua sekta ya madini inaweza kutoa mchango mkubwa kwa Taifa hili.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here