Rais Magufuli ampa ahueni Sugu

0

NA MWANDISHI WETU, DAR

RAIS Dk. John Magufuli amemuhakikishia aliyekuwa mbunge wa Mbeya mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kuwa hoteli yake haitobomolewa kwa kuwa imefuata taratibu zote.

Katika siku za hivi karibu kulikuwa na uvumi kwamba hoteli hiyo itabomolewa kwa kudaiwa kujengwa kwenye chanzo cha maji.

Akizungumza katika moja ya video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila akiwa na Mbilinyi alisema Rais Magufuli amemtuma aeleze kwamba mtu yeyote hatakiwi kusema anabomoa hoteli hiyo.

“Kwa sababu huyu ni mwekezaji kama wawekezaji wengine na ikiwezekana amedai kama tuna viwanja vingine upande huu wa uzunguni basi moja ya watu wanaotakiwa kufaidika navyo ni pamoja na Sugu ambaye amekwisha ananza kuwekeza hapa.”

“Hoteli hii ilianza kupimwa ardhi maana yake ardhi hii imepimwa na ina hati, watu wa mipango miji na wanaohusika na upimaji walishapima maana yake hadi mkurugenzi wa ramani anafahamu eneo, sasa kama umetoa hati kwenye eneo lenye chanzo cha maji na leo unategemea baada ya kusimika hoteli ulitaka iweje, kwahiyo vibali vyote vilifuatwa mlolongo wake, ” alisema Chalamila.

Aliongeza, “Mmeona anatunza maji vizuri na maji yanatirika vizuri na hayajakakuka. Inawezekana hoteli nyingine ambazo zimekausha maji sio hii, inawezekana ni za wana CCM ndiyo ziunakausha maji, suala hili lisipelekee mvurugano wa kisiasa, mimi kauli yangu nasema maji ataendelea kuyatunza kama mnavyoona.”

“Hoteli hii watu wa NEMC wanaijua, watu wa OSHA wanaijua, watu wa halmashauri wanaijua, mkuu wa mkoa anaijua, TRA wanaijua sasa kama wote tunaijua leo iweje tuseme iko kwenye maji, wakati inajengwa walikuwa wapi, wakati tunapima ardhi ilikuwa wapi au mto haukuwepo umekuja leo.” Alihoji Chalamila.

Kwa upande wake Sugu alisema kuwa anaamini ujumbe uliobebwa kwenye salamu za Rais utasaidia kuleta kujiamini hata kwa wafanyabiashara wengine, kama itatokea nafasi ya kuwekeza zaidi Mbeya.

Alisema yeye binafsi hakuwa na hofu kwasababu alikuwa na nyaraka zote zilizompa uhalali wa kujenga Hoteli eneo hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here