Rais Magufuli afurahishwa na kasi waliyoanza nayo mawaziri

0

Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameonyesha kufurahishwa na kasi waliyoanza nayo Mawaziri wake katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni wiki moja tu tangu awaapishe na kuwapa maelekezo mbalimbali.

Mara baada ya kuapishwa mawaziri hao walianza kazi mara moja ambapo tulishuhudia wakitembelea maeneo yao ya kazi na kutoa maelekezo mbalimbali kwa watendaji wa taasisi zao. Pia wapo ambao hawakuridhishwa na ufanyaji kazi wa baadhi ya watendaji na kuagiza waondolewe katika nafasi zao.

Mawaziri pia walianza kutembelea miradi iliyopo chini ya wizara zao kujionea namna inavyotekelezwa na kutoa maelekezo mbalimbali ikiwemo wakandarasi kuhakikisha inakamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.

Ni dhahiri kwamba kasi hiyo ya mawaziri imemvutia Rais Magufuli ambapo jana wakati akiwakaribisha katika kikao cha kwanza cha Baraza la Mawaziri kilichofanyka Ikulu jijini Dodoma aliwaambia kuwa wameanza vizuri.

“…karibuni basi tuanze kikao chetu tumeona leo tukutane hapa wote tutoe mwelekeo lakini kwa ujumla mmeanza vizuri sana, hongereni sana…” alisema Rais Magufuli.

MAWAZIRI WALIANZA NA MOTO

Mara baada ya kuwaapisha Rais Dk. John Magufuli aliwataka Mawaziri  kwenda kushirikiana na Manaibu wao kufanya kazi kwa bidii na kufanya maamuzi katika utekelezaji wa mipango iliyopo.

Rais Magufuli pia alisema hatosita kumwondoa yeyote ambaye hatoleta matokeo chanya katika utendaji kazi wake na kuanisha yale anayotarajia katika kila wizara.

Mbali na Rais Magufuli pia Waziri Mkuu alikutana nao mara baada ya kuapishwa kwa lengo la kupeana maelekezo ya kile kinachotakiwa kufanyika katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Huenda maelekezo hayo ndiyo imekuwa chachu ya mawaziri hao kuanza mara moja kutembelea maeneo yao wakiwa na Manaibu wao kwaajili ya utambulisho na kupeana maelekezo ya namna bora ya utendaji kazi.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso yeye alianza kwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Dodoma (Duwasa), David Palangyo na kumtaka asubiri kupangiwa kazi nyingine.

Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk. Faustine Ndugulile alikutana na Menejimenti ya Wizara hiyo akiwa na Naibu wake Mhandisi Kundo Andrea Mathew kwa lengo la kufahamiana na kutoa maagizo juu ya utendaji kazi ili Wizara hiyo mpya isimame na kuchukua nafasi yake katika utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi na kueleza kuwa anataka Tanzania iwe na uchumi wa kidigitali.

Waziri wa Madini Doto Biteko, alifuta leseni Sita za wafanyabiashara wa madini ya dhahabu ambao wanatuhumiwa kujishughulisha na utorashaji wa madini wilayani Chunya. Rais Magufuli katika hotuba yake siku ya kuwaapisha aligusia suala hilo.

Vile vile Waziri Biteko aliwasimamisha kazi watumishi watatu wa Ofisi ya Madini wa Mkoa wa kimadini wa Chunya baada ya kutuhumiwa kushirikiana na wafanyabiashara kutorosha madini.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu aliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini kutokuwa kikwazo katika utoaji wa vibali vya mazingira kwa wawekezaji katika kutekeleza miradi ya kimkakati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here