Rais Magufuli aahirisha sherehe za Uhuru

0

   >>Aagiza Sh. 835 Mil. zilizokuwa zitumike, kununulia vifaa Hospitali mpya ya Uhuru iliyojengwa Dodoma

NA MWANDISHI WETU

RAIS Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara zilizotarajiwa kufanyika Desemba 9, 2020 na kuelekeza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kununulia vifaa mbalimbali kwa ajili ya Hospitali ya Uhuru.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Dk. Magufuli ameagiza kiasi cha Sh. 835,498,700 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe za maadhimisho ya 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara zitumike kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya hospitali hiyo.

Waziri Mkuu alitoa taarifa hiyo kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) zilizofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Alisema Rais Dk. Magufuli aliagiza siku hiyo itumike kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii nchini.

Itakumbukwa kuwa Novemba 20, 2018, Rais Dk. Magufuli aliagiza kiasi cha sh. 995,182,000.00 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara 9 Desemba, zitumike kujenga Hospitali ya Uhuru, ambayo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 92.

Itakumbukwa mwaka 2018 aliagiza Sh Bilioni 995.1 za Sherehe za uhuru zitumike kuanza kujenga Hospitali hiyo ambayo ujenzi wake sasa umefikia asilimia 92.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa mwaka huu inasema; ‘Miaka 59 ya Uhuru na Miaka 58 ya Jamhuri: Tanzania yenye Uchumi Imara Itajengwa na Watanzania Wenyewe, Tufanye Kazi kwa Bidii, Uwajibikaji na Uadilifu.’

Waziri Mkuu alisema hadi kufikia sasa ujenzi wa hospitali hiyo ya Uhuru umegharimu shilingi bilioni 4.2.

Itakumbukwa pia Januari 2019 wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya Simu ya Airtel Rais Dk. Magufuli aliagiza kiasi cha shilingi bilioni 2.4 zilizotolewa na kampuni hiyo zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here