PURA katika mapinduzi ya kiuchumi

0

Na Hafidh Kido

MARA kwa mara katika hotuba zake Rais Dk. John Magufuli amekuwa akikariri maneno ya kuonyesha anahitaji Watanzania wanufaike na rasilimali zao hasa madini na gesi asilia.

Anasema, sisi si masikini kwa kuwa tuna vitu ambavyo wengi hawajapewa na pengine ndiyo sababu baadhi ya mataifa ya kimagharibi hayavutiwi na maendeleo yanayopatikana nchini, wanasababisha chokochoko za kutuvuruga.

Mwaka 2019 Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani akiwa katika kongamano la siku tatu la kuhamasisha uwezeshaji na uwekezaji katika shughuli za utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi alisema Tanzania imefungua mikono yake kuwataka wawekezaji waje kwa kuwa
rasilimali hiyo ipo kwa wingi.

Aidha, kongamano hilo lililofanyika kuanzia Oktoba 2-3, 2019 jijini  Dar es Salaam, lilihudhiriwa na watu zaidi ya  500 kutoka mataifa 67 duniani.

“Kila mmoja ni shahidi, mafanikio ya sekta Gesi hivi sasa yameongezeka ambapo mwaka jana (mwaka juzi 2018), gesi ilichangia asilimia 2 ya pato la taifa, kutoka asilimia 0.9 mwaka 2017, ongezeko hili pia linatokana na kazi ya usambazaji na uuzaji wa gesi hiyo kutoka kwenye uzalishaji kwenda kwa watumiaji, hakika haya ni mafanikio makubwa.”

Aliongeza kuwa matumizi ya gesi yameongezeka kutoka kipimo cha ujazo wa gesi futi Milioni 45( mmsf) mwaka 2013/14 , hadi kufikia Milioni 110 mwaka 2019 kwa ajili ya
kuzalisha umeme, pia futi za ujazo takribani Milioni 70, zinatumika kwa ajili ya matumizi mengine ya ndani ikiwepo katika magari pamoja na viwanda.

Kwa miaka 15 iliyopita hadi sasa, Matumizi ya gesi ni takribani asilimia 1 ya kipimo cha ujazo wa Trilioni 57.54 ya gesi yote iliyogunduliwa nchini, matumizi hayo yanaendelea kuongezeka kutokana na kuwepo na miundombinu ya kuzalisha umeme unaotumia gesi,
pamoja na mahitaji ya matumizi mengine ya gesi kuongezeka.

Alisema bado shughuli za utafiti zinaendelea ili kupata gesi nyingi zaidi kwa matumizi ya Watanzania katika miaka ijayo.

Takribani asilimia 55 ya umeme unaotumika nchini unazalishwa kwa kutumia rasilimali ya gesi. Matumizi ya gesi ni nafuu kwa asilimia 40 ya matumizi ya kuni na mkaa na kuhifadhi mazingira, takribani magunia 5,000 ya mkaa hutumika kila mwaka kwa mkoa wa Dar es salaam pekee, hivyo gesi hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa katika utunzaji wa mazingira.

Hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), ilikuwa na semina kwa wanahabari kuzungumza nao na kujadiliana juu ya hali ya rasilimali hiyo nchini, ambapo miongoni mwa watoa mada alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni aliyewapitisha wanahabari katika historia ya utafutaji mafuta na gesi asilia nchini, alisema:

“Shughuli za utafutaji mafuta na gesi asilia nchini zilianza miaka ya 1950 kupitia Kampuni ya Agip kutoka Italia. Licha ya shughuli hizo kuanza miaka ya 1950, Kampuni ya Agip ilifanya ugunduzi wa kwanza katika Kisiwa cha Songo Songo(Lindi) mwaka 1974 ambao ulifuatiwa na ugunduzi mwingine katika eneo la Mnazi Bay (Mtwara) mwaka 1982.

“Hata hivyo, gesi asilia hiyo haikuendelezwa kwa kuwa ilionekana haina manufaa ya kiuchumi (uneconomical) kwa wakati huo. Baada ya ugunduzi huo, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) iliendelea kufanya utafiti ikiwa ni pamoja na kuchimba visima mbalimbali kwa ajili ya kuthibitisha kiasi cha gesi asilia kilichopo katika maeneo ambako gesi asilia iligunduliwa. Hadi Novemba, 2014 kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa nchini ni futi za ujazo trilioni 53.28.”

Mhandisi Sangweni alibainisha, hadi sasa kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa nchini ni futi za ujazo trilioni 57.54, ambacho kinaweza kutumika kwa miaka mingi zaidi na kukumbusha kuwa kinachotumika kwa sasa ni asilimia ndogo tu ya utajiri uliopo ardhini na majini.

Akizungumzia uanzishwaji wa PURA, Mhandisi Sangwini alisema mamlaka hiyo iliundwa kupitia kifungu namba 11, cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2015.

“Sababu za uanzishwaji wake ni pamoja na: Ugunduzi mkubwa wa gesi asilia kwenye kina kirefu cha bahari. Uhitaji wa uimarishaji wa mifumo ya kisheria, kitaasisi na udhibiti. Kutenganisha majukumu ya kibiashara na udhibiti wa sekta ya petroli nchini na  kuendana na mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa sekta ya mafuta duniani,” alisema Mhandisi Sangwini na kufafanua:

“Majukumu ya PURA yameainishwa katika Sheria ya Petroli ya 2015, kifungu Na. 12 na kwa ujumla wake yamegawanyika katika makundi makuu matatu ikiwemo: kuishauri Serikali juu ya masuala mbalimbali yahusuyo Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji wa mafuta au gesi asilia;

“Kusimamia na kudhibiti shughuli zote zinazohusiana na mkondo wa juu wa petrol; na  kusimamia utekelezaji wa mradi wa kuchakata gesi asilia kuwa katika mfumo wa
kimiminika (Liquefied Natural Gas Project). Ambapo majukumu haya yameainishwa zaidi kwenye kifungu cha 12 (2), ambapo yanazalisha majukumu 18 kwa ujumla wake.”

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia kutoka Madimba-Mtwara, Songo Songo – Lindi na Pwani hadi Dar es Salaam ya Machi, 2015 inaeleza kuwa Tanzania imeamua kutumia gesi asilia kuzalisha umeme kwa sababu mbalimbali ikiwamo;

Kupunguza utegemezi wa umeme unaozalishwa kwa kutumia maji (Hydropower) ambao unaathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kama ukame, vilevile kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje kwa ajili kuzalisha umeme.

Sababu nyingine ni kushirikisha sekta binafsi katika sekta ya nishati na kuvutia wawekezaji katika shughuli za utafutaji mafuta na gesi asilia nchini.

Ambapo, imebainika utekelezaji wa mradi huu utaiwezesha nchi kupata umeme wa uhakika na wa bei nafuu.

Itakapokamilika miundombinu hiyo itaokoa zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 1 sawa na  shilingi Trilioni 1.6 kwa mwaka, zinazotumika sasa kuagiza mafuta kwa ajili ya kufua umeme kwa kutumia mitambo ambayo tayari ipo nchini.

Kadhalika mitambo mipya inayojengwa itapata gesi asilia kuzalisha umeme wa bei nafuu.

Aidha, hadi sasa Shirika la Umeme Tanesco kupitia gridi ya taifa inazalisha Megawati 1,565.72 na umeme utokanao na gridi ya taifa na vyanzo vilivyo nje ya gridi ni Megawati 1,601.84, ambapo asilimia 86.5 ya umeme unaozalishwa nchini unamilikiwa na Tanesco.

Hii ni mbali ya Megawati 2115 zitakazozalishwa baada ya kukamilika mradi mkubwa wa Julius Nyerere (JNHPP). Mahitaji kwa sasa ni Megawati 1,177.20.

Aidha, umeme unaozalishwa kwa kutumia gesi asilia nchini ni Megawati 703.72 kutoka  katika mitambo mbalimbali nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here