PUMZIKA MWAMBA

0

Na MWANDISHI WETU

JANA saa 10:50 ilikuwa simanzi na majonzi kwa Watanzania wote wakati jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dk. John Magufuli lilishushwa katika nyumba yake ya milele na kufuatiwa na tukio la ndugu, jamaa na marafiki kuweka udongo.

Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo.

Shughuli ya maziko iliyofanyika kijiji cha Mlimani wilayani Chato Mkoa wa Geita katika makaburi ya familia  ilihusisha watu wachache wakiwemo viongozi wa Serikali, wastaafu na familia yake mara baada ya kumalizika kwa ibada ya misa ya kumwombea iliyofanyika katika uwanja wa Magufuli.

Majonzi, simanzi na huzuni vilitawala makaburini hapo wakati mwili wa kiongozi huyo ukishushwa kaburini.

Shughuli za maziko ya Rais Magufuli zilifanyika kwa desturi ya kanisa katoliki na kisha baadae zilifanyika taratibu za kijeshi ambapo kulifanyika gwaride la heshima mbele ya kaburi na kupigiwa mizinga 21.

 Awali akitoa salamu za pole mara baada ya ibada ya misa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliongoza maelfu ya waombolezaji katika maziko hayo, aliwashukuru makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, vyombo vya habari na wanasiasa  kuwa bega kwa bega na Serikali tangu kutangazwa kifo cha Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Magufuli hadi leo Ijumaa Machi 26, 2021 siku anayopumzishwa katika nyumba yake ya milele.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi alitoa shukrani hizo leo Ijumaa Machi 26, 2021 kupitia ukurasa wa mtandao wake wa  kijamii wa Instagram.

“Leo tunapompumzisha mpendwa wetu Hayati Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli kwenye nyumba yake ya milele, kwa niaba yangu binafsi na niaba ya watu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kuwashukuru Watanzania wenzangu, Viongozi wenzangu pamoja na Viongozi Wastaafu.”

“Viongozi wa Nchi na Mashirika Mbalimbali ya Kimataifa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kisiasa, Jumuiya ya Kidiplomasia, Vyombo vya Habari, wasanii na kila aliyekuwa nasi bega kwa bega wakati huu mgumu kwa Taifa letu. Tafadhali pokeeni shukrani zetu za dhati na muendelee kuiombea roho ya Hayati Dk  Magufuli ipumzike kwa amani na Mungu aendelee kuifariji familia yake,” alisema

Aidha  Rais Samia aliwahakikishia wakazi wa Wilaya ya Chato kuwa ahadi iliyotolewa na Hayati John Magufuli  ya Wilaya hiyo kuwa Mkoa inafanyiwa kazi.

“Niwahakikishie  wakazi wa Chato kuwa tutatekeleza ahadi zote alizotoa kwa watu wake na zote zilizopo kwenye ilani ya CCM. Kuhusu Chato kuwa Mkoa nina   taarifa mchakato umeanza hivyo nawataka mwasilishe serikalini hatua za mchakato huo ili kuangalia kama umekidhi vigezo vya kuwa Mkoa.”

“Kama vigezo vimekidhi tutalikamilisha hilo, kama havijakidhi tutawashauri namna ya kufanya ili vikidhi. Leo nipo Chato mara ya tatu, mara ya kwanza nilikuja kwenye kampeni 2015, mara ya pili wakati wa msiba wa dada yake Magufuli. Mara ya mwisho nilipokuja Chato alinionyesha eneo la kaburi ya familia, sikuwaza kwamba ndani ya muda mfupi nitakuja kwa ajili yake kwenye eneo lile lile,” amesema Rais Samia.

KIKWETE: MAGUFULI ALIKUWA CHAGUO LANGU LA KWANZA

Akitoa salamu za pole Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alielezea namna alivyokuwa karibu na Rais Magufuli na kudokeza kuwa yeye ndiye alikuwa chaguo lake la kwanza wakati wa mchakato wa kumpta mgombea urais mwaka 2015.

Kikwete alisema alikuwa pendekezo lake la kwanza kati ya majina matano aliyoyapeka Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwaajili ya kupigiwa kura.

“Waswahili wanasema akutukane hakuchagulii tusi unaposikia minong’ono kwamba unasikia Kikwete hakumtaka Magufuli mimi labda Kikwete mwingine nimewasimulia leo mchakato tulivyokwenda na  yale majina matano nilikuja nayo mimi tumepambana nayo mpaka yakatoka na la kwanza lilibaki kuwa la JPM nililoliweka mie  nashukuru kwenda hadi mkutano mkuu ikawa hivyo hivyo.”

“Oooh… Kikwete anamchukia Magufuli eeh labda mwingine si mimi, namchukiaje mtu uliyemkabidhi  ilani  ya uchaguzi  na ameitekeleza kwa kiwango cha juu sana lakini nikasema dunia waganga njaa wengi wanapata ulaji wao kwa kuongopa,” alisema Kikwete.

Aidha alisema alisema alimuamini zaidi rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli na ndio maana alimteua kuwa waziri katika wizara tatu tofauti katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake akisema, “alikuwa jembe langu.”

Kikwete ambaye kwa nyakati tofauti alimteua Magufuli kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ujenzi alisema kiongozi huyo alikuwa jembe lake alilolitegemea ndiyo   maana alimuweka  kwenye wizara tatu ngumu.

“Nilianza na wizara ya ardhi nilimwambia kule kuna wala rushwa, wanagawa viwanja mara nne nne, wale ni watu wagumu mno nikamwambia akawanyooshe.”

“Akaenda kufanya kazi kubwa akawanyoosha, akajitahidi lakini wale watu ni wagumu mno, Rais ukifanikiwa kuibadilisha wizara ya ardhi watu watashukuru,” alisema.

Alisema baada ya kufanya kazi hiyo vizuri alimuhamishia wizara ya mifugo ambako nako aliiendesha vyema wizara hiyo.

Kikwete alieleza kuwa katika miaka mitano ya mwisho ya uongozi wake alimuhamishia Magufuli wizara ya ujenzi ili aweze kuiunganisha mikoa yote kwa barabara za lami.

“Miaka mitano ya mwisho nilitaka kufanya kitu ambacho kitaacha alama na niliona kuunganisha mikoa ndiyo kitu muhimu nikamkabidhi kazi hiyo Magufuli.”

“Tumeona sasa hivi mikoa karibu yote imeunganishwa kwa barabara kama imebaki ni michache, alifanya kazi hiyo kwa ufanisi,” alisema Kikwete.

Pia alitumia fursa hiyo kueleza namna anavyomwamini Rais Samia kwa kusema kuwa ni mtu sahihi na ataendeleza kazi aliyoiacha mtangulizi wake Hayati John Magufuli.

Alisema viongozi wastaafu wapo tayari kumpa kila aina ya ushirikiano endapo atahitaji msaada wao.

“Mimi na wastaafu wenzangu tutakuwa pamoja na wewe, tutume tutakuitika usipotutuma tutaendelea na shughuli zetu,” amesema Kikwete.

Akizungumzia hotuba ya Rais Samia baada ya kuapishwa, Kikwete alisema imewafariji na kuwafuta machozi Watanzania.

 “Nilipata bahati ya kusikiliza hotuba yako umetufuta machozi muhimu zaidi umetuhakikishia kuwa nchi yetu ipo katika mikono salama na hakuna litakaloharibika.”

 “Binafsi sina mashaka na uongozi wako kwa sababu nakufahamu, nimekufahamu zaidi ulipokuwa waziri wangu ukiwa waziri wa nchi unayeshughulikia muungano. Kama uliweza kushughulikia yale ukiwa waziri tunategemea makubwa zaidi ukiwa rais. Kipaji chako ulichoonyesha kwenye Bunge la katiba ilitudhihirishia uwezo wako wa uongozi na ni sababu hiyo chama kikakuteua kuwa mgombea mwenza.”

“Unayajua vyema matarajio ya wana CCM na matarajio ya Watanzania kwa Serikali yao, wewe ni mbobevu uliyepikwa ukapikika,” amesema Kikwete.

SHEIN ASIMULIA MIAKA 19 ALIYOFANYA KAZI NA MAGUFULI

Rais wa Zanzibar aliyemaliza muda wake, Dk. Ali Mohammed Shein alitoa simulizi ya miaka 19 na nusu aliyofanya kazi na aliyekuwa Rais wa tano wa Tanzania, Dk John Magufuli huku akisema kiongozi huyo alikuwa na maono ya mbali.

“Nimeishi na kufanya naye kazi miaka 19 na nusu. Miaka tisa na nusu nikiwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na miaka 10 nikiwa rais wa Zanzibar, nina mengi sana niliyoyaelezea niliyoyaona hususan kuimarisha muungano wetu,” alisema Dk Shein.

Alisema kati ya sifa kubwa Magufuli alikuwa mkweli wa dhati, muungwana na ukweli wake haogopi binadamu mwenzie bali anamuogopa Mungu.

“Anayoyasema ndiyo anayoyafanya, wengi wanadhani yeye ni mkali ila si kweli, bali kiongozi lazima aongoze katika misingi ya haki na usawa ameyafanya hayo kwa vitendo wengi tumeshuhudia,” alisema.

Dk Shein alisema Magufuli anaweza kuona mbali zaidi, “Ninachokumbuka namna anavyoona mbali, siku alinialika nikiwa Makamu wa Rais tukaizindue barabara Tegeta kwenda Bagamoyo yeye alikuwa waziri. Akaninong’oneza jambo sikuamini unaona barabara hii itakwenda kusini na kaskazini lakini mpaka leo naamini amefanya zaidi ya pale alipopasema.

 “Nilikuwa namuamini sana katika Muungano alinitia moyo sana alikuwa ananiambai tufanye kazi watu wataona wenyewe. Niseme tu Rais Samia wengi tunamfahamu uwezo, uchapakazi, imani yako na namna ulivyokuzwa, tunaamini utatufikisha.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here