PST YAUNDA KAMATI KUCHUNGUZA KUFUTWA MIKANDA YA MABONDIA WA TANZANIA

0

>Wamo Hassan Mwakinyo naTwaha Kiduku

NA SHEHE SEMTAWA

MABONDIA wa Kitanzania waliopigana michezo ya kimataifa kuwania mikanda ndani ya ardhi ya Tanzania kuanzia mwaka 2018, mapambano yao yamefutwa na hayatambuliki kimataifa.

Hatua hiyo, inakuja baada ya kudaiwa kuna ubabaishaji kwa mabondia wanaoletwa kupigana Tanzania kuwa wana ushindani mdogo na wako chini ya viwango kimataifa.

Miongoni mwa mapambano hayo, yaliyofutwa ni pamoja na la Hassan Mwakinyo dhidi ya Arnel Tinampay wa Philippines na lile la Twaha Kassim ‘Kiduku’ na Sirimngkhon Lamthuam kutoka Thailand.

Akizungumzia tukio hilo la kukatisha tamaa kwa mabondia wa Tanzania, Katibu Mkuu Shirikisho la mchezo wa Ngumi za Kulipwa nchini (PST), Anton Luther, alikiri kuwa ni kweli mapano hayo, kuanzia mwaka 2018 hadi 2020 yamefutwa.

“Yani maana yake inaonesha kuwa bondia aliyeanza kupanda mwaka 2018 mpaka leo hana mkanda na madhara yake ni kwamba, kama mapambano yanafutwa maana yake wewe huna rekodi nzuri hata ya kwenda kucheza kokote.

“Kwa sababu ngumi za kulipwa tunaangalia rekodi ya bondia huwezi ukaniambia kuwa una bondia atakuja kucheza halafu namtafuta kwenye mtandao wa rekodi za mabondia na kuta ana mapambano matatu au manne tu.

“Sifa kubwa ni kwamba lazima uwe na mapambano ya kutosha na umeshinda mangapi, umepigwa mangapi sasa inapotolewa kwa hiyo inakuwa ni tatizo kubwa,”alisema Luther.

Kutokana na mazingira hayo, Luther alisema wamo kwenye mchakato wa kuunda Kamati ambayo itafanya kazi ya kufuatilia mkanganyiko huo.

“Lakini bado vile vile…Ah! Niseme kamati tayari imeishaundwa na ndani ya siku nne tano wiki hii mpaka Ijumaa tutakuwa tumesha kuja na majibu.

“Lakini taarifa hizi bwana ni za kweli na nijanga kubwa mno kwa mabondia wa Taifa letu la Tanzania kwa sasa,”alisema Luther.

Akifafanua zaidi, Luther alisema “Sababu inawezekana kuna mambo mawili ambayo yanaweza yakajitokeza kwa sababu inawezekana sisi wenyewe kwa wenyewe tunazunguukana mtu anafanya hivi na mwingine anafanya hivi ni kama vile hampendani.

“Kwa hiyo mtu anaamua anakuchomea kwa staili moja ama nyingine, huyu anamchomea kwa staili nyingine lakini tusihukumu inawezekana hata huko nje, mapambano kwa hao wenzetu hawachezi kuna lockdown.

“Inawezekana vile vile hata wao hawaridhiki, manaake  sisi tukicheza mabondia wetu wanaenda juu.

“Kama mtakumbuka hivi karibuni bondia wetu Hassan Mwakinyo alishushwa viwango lakini si kama alipigana ulingoni bali ni kwa sababu alikaa muda mrefu bila kucheza,”alisema Luther.

Aidha, Luther, alisema kuwa hata wazungu kwa muda mrefu sasa hawajacheza kwa hiyo kucheza kwao kunawafanya wazidi kupanda juu katika ubora wa viwango.

“Kwa hiyo unaweza ukakuta penine ni vita ya kiitelejensia katika masumbwi ya kidunia na wazungu na sisi au la, lakini pote pote lakini tumeunda kamati itakuja na majibu sahihi ndani ya Wiki moja,”alisema Luther.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here