Prof. Manya ateuliwa Naibu Waziri wa madini mpya akichukua nafasi ya aliyeshindwa kuapa

0

Na Mwandishi Wetu 

Rais wa Tanzania,  John Magufuli amemteua Profesa Shukrani Manya kuwa naibu waziri wa Madini ikiwa ni baada ya kumteua kuwa mbunge.

Uteuzi wa Profesa Manya umekuja ikiwa zimepita siku mbili tangu kiongozi mkuu huyo wa nchi kusema kuwa atateua mbunge mwingine kuwa waziri baada ya aliyemteua awali, Francis Kumba Ndulane ambaye ni mbunge wa Kilwa Kaskazini kushikwa kigugumizi wakati akila kiapo.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Desemba 11, 2020 na mkurugenzi wa mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa kabla ya uteuzi huo  Profesa Manya alikuwa katibu mtendaji wa tume ya madini Tanzania.

Inaeleza kuwa uteuzi wa Profesa Manya unaanza leo na ataapishwa leo mchana Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.

Desemba 9, 2020 Rais Magufuli wakati akiwaapisha mawaziri 21 na manaibu waziri 22, ilitokea rekodi baada ya mteule wa nafasi ya naibu waziri kuhangaika kusoma kiapo hadi kutakiwa akapumzike na baadaye Rais kutangaza kufanya uteuzi mpya.

Kama haitoshi, Rais aliahidi kuangalia upya wasifu wake licha ya kuelewa awali kuwa wakati wa uteuzi walichambua kila mmoja na mambo mengine kadhaa.

Mteule aliyehangaika kusoma kiapo na kupewa nafasi ya kujisahihisha mara mbili alikuwa Ndulane ambaye kama si tatizo hilo angekuwa akitembelea gari la Naibu Waziri wa Madini, ambalo lililazimika kurudi bila ya bosi.

Ndulane, mwenye elimu ya shahada ya uzamili, alikuwa miongoni mwa wateule wachache waliokosea kusoma kiapo hicho wakati wa hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Akizungumza baada kuwaapisha mawaziri wote, Rais Magufuli alisema alipitia CV ya kila waziri aliyemteua akiwamo Ndulane na kujiridhisha ana sifa. Hata hivyo, alisema nafasi hiyo atapewa mtu mwingine na yeye ataendelea na nafasi yake ya ubunge.

“Tutamteua mtu mwingine anayeweza kuapa vizuri. Tunakupongeza, utaendelea kuwa mbunge lakini lazima tutafute replacement (mbadala) yako.”

Rais Magufuli alisema wataiangalia vizuri shahada yake ya uzamili, akitoa mifano ya watu ambao wamekuwa ‘wakichomekea’ sifa za kielimu ambazo hawana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here