Ponda apondwa kila kona

0

NA DOTTO KWILASA,DODOMA

BARAZA Kuu la Waisalamu Tanzania (Bakwata) limelaani vikali  kauli iliyotolewa na Sheikhe Issa Ponda kwamba waisalamu nchini  wamekubaliana kumpigia kura  Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Hatua hiyo imekuja kufuatia Oktoba 17 mwaka huu katika mkutano wa kampeni wa kumnadi Lissu  uliofanyika katika uwanja wa shule ya Msingi Uhuru Jijini hapa ambapo Sheikhe Ponda alisema kwamba Waislamu wamekubaliana kwamba kura zote ni kwa Lissu na si vinginevyo.

Akizungumza jana Jijini hapa na Waandishi wa Habari, kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikhe Abubakari Zubeir, Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu alisema kauli iliyotolewa na Ponda ni  ya kwake   peke yake na si ya waislamu.

“Tamko  lilotolewa na Sheikhe Issa Ponda,katika mkutano ambao ulifanyika na chama fulani hapa Dodoma kuhusiana na kauli aliyoitoa kuwaambia Waislamu wa Tanzania kwamba eti waislamu wote wamekubaliana kwa ujumla wampigie kura mgombea wa chama hicho.

“Tunapenda kuufahamisha umma kuwa,kauli hii ni  yake yeye mwenyewe hakuna mwislamu popote wala sehemu yoyote wala kikao chochote walichokaa na kukubaliana kwamba eti wakipe kura chama fulani au mgombea fulani kama alivyoeleza Ponda.

“Haya maneno yapuuzwe sio sahihi ni maneno ambayo mtu ameyazunguza kwa maslahi yake kwahiyo maneno haya yanaashiria uvunjifu wa amani yale maneno anatakiwa achukuliwe hatua za kisheria kwa sababu moja kwa moja anahamasisha watu vurugu ama uvunjifu wa amani kwa sababu kuna maisha baada ya uchaguzi na kuna kushinda na kushindwa,”alisema.

Sheikhe Rajabu alisema wanakemea tamko hilo na kwamba msemaji wa mambo ya Bakwata ni Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikhe Zubeir.

“Halazimishwi mtu yoyote kuwa upande wa chama fulani yale maneno tunarudia kusema yale maneno yapuuzwe kwa sababu msemaji wa Bakwata ni Mufti Mkuu wa  Tanzania Abubakri Zubeir na wala sio Sheikhe Ponda kwani hajulikani ni kiongozi wa Taasisi gani au ni mwalimu wa Madrasa gani sisi hatumtambui,”alisema.

Alisema hivi karibuni   Baraza la Masheike Mkoa wa Dodoma lilikaa kikao ambapo   agenda walizokubaliana ni kuwakumbusha viongozi wa dini wajibu wao wakati wa kipindi hichi cha kampeni.

“Lakini pia mbaya zaidi katika agenda ambazo tumekubaliana ni kuwakumbusha viongozi wa dini wajibu wao kwa sababu toka tuanze kampeni hizi za kuingia katika uchaguzi kumekuwa na maneno ya viongozi wa dini ambayo yanaleta ukakasi.

“Ambayo yanasababisha mtafaruku  lakini mengine kuelekea uvunjifu wa amani sisi kama viongozi wa dini tunatakiwa tusijihusishe na chama chochote cha siasa na ndio makubaliano yetu hata katika kamati zetu za amani katika Mikoa yote hapa nchini.

“Kutokujihusisha na kupigia kampeni chama chochote bali kila kiongozi anautashi na chama anachokitaka yeye.

“Hakuna kulazimishana kwamba uwe dini fulani ama chama fulani sisi ni walezi wa vyama vyote wanapokea tuwasuluhishe, lakini kujihusisha moja kwa moja na kutenda mema.

“Hili kama viongozi wa dini tunalikemea na tuliishakubaliana, sasa mbaya zaidi viongozi wa dini wanasimama kabisa katika majukwaa ya vyama vya siasa katika viwanja kutoa matamko na kuhamasisha wananchi wamchague mtu fulani ama wachague chama fulani.

“Hili jambo tunawashauri na kuwanasihi viongozi wetu wa dini warudi kwenye makubaliano yetu hayo sio makubaliano yetu tukifanya hivyo  viongozi wa dini tutakuwa ni sehemu yenye kupelekea katika viashirifu  vya uvunjifu wa amani.

“Tunahamasisha watanzania waende wakapige kura na kuchagua kiongozi yeyote wanayeona anafaa kwa maslahi ya Taifa,”alisisitiza .

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here