Nyota wa 5 Simba hatihati kuwakosa Ruvu Shooting

0

NA MWANDISHI WETU

MAMBO ni magumu kwa Klabu ya Simba kutokana na kuandamwa na wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza kusumbuliwa na majeraha ambapo wanatarajiwa kukaa nje kwa muda wa wiki tatu huku wengine wakiwa wameanza mazoezi mepesi kurejea kwenye ubora wao.

Ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake 13 baada ya kucheza mechi sita na kufunga mabao 14, leo Jumatatu inatarajiwa kuwakosa mastaa wake watano ambao wanasumbuliwa na majeraha.

Mastaa hao ambao wapo kikosi cha kwanza ni pamoja na:-Meddie Kagere, Gerson Fraga, John Bocco, Shomari Kapombe, Chris Mugalu.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, Kagere mwenye mabao manne atakaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki tatu.

Tayari ameshakaa nje ya uwanja kwa muda wa wiki moja na kwa sasa amebakiza wiki mbili hivyo anatarajiwa kurejea uwanjani kuanza mazoezi Novemba 6, hivyo kuna hatihati ataukosa mchezo wa Yanga Novemba 7.

John Bocco ambaye ni nahodha mwenye bao moja kwa sasa bado hajarejea kwenye ubora wake akiendelea kutibu majeraha aliyoyapata kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye sare ya kufungana bao 1- 1 Uwanja wa Jamhuri.

Fraga pia Septemba 23 taarifa rasmi kutoka Simba ilieleza kuwa atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki tatu ama wiki nne kwa kutibu mguu wa kushoto, tayari wiki hizo alizopewa zimeisha hivyo kwa sasa ameanza mazoezi mepesi kabla ya kurejea uwanjani.

Mchezaji huyo aliumia kwenye mchezo dhidi ya Biashara United wakati Simba ikishinda mabao 4-0 pale Uwanja wa Mkapa.

Shomari Kapombe, beki wa kulia wa Simba yeye aliumia kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons Oktoba 22 wakati timu ikipoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Kwa mujibu wa daktari wa timu ya Simba, Yassin Gembe, taarifa rasmi itatolewa hivi karibuni

Chris Mugalu naye pia yupo kwenye uangalizi baada ya taarifa kueleza kuwa alitonesha nyonga walipokuwa kwenye maandalizi ya mwisho dhidi ya Tanzania Prison.

Leo Oktoba 26 saa 10:00 Simba ina kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya Ruvu Shooting ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons huku Ruvu Shooting ikiwa imetoka kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na KMC.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here