Ntibazonkiza aanza kuweka rekodi za kutisha

0

NA MWANDISHI WETU

NYOTA mpya wa Yanga, Saido Ntibazonkiza ameweka rekodi yakee ndani ya ardhi ya Tanzania baada ya kufunga jumla ya mabao matatu na pasi moja kwenye mechi zake mbili za mwanzo.

Ingizo hilo jipya kwenye usajili wa dirisha dogo kutoka nchini Burundi alianza kufanya makeke kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Singida United.

Mchezo huu ulikuwa ni wa kirafiki na matokeo ilikuwa Yanga 3-0 Singida United, Uwanja wa Liti ambapo alifunga mabao mawili, moja kwa penalti.

Mwishoni wa wiki katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na matokeo yalikuwa Yanga 3-1 Dodoma Jiji alitupia bao moja kwa faulo na pasi moja ambayo alipiga pia kwa njia ya faulo.

Rekodi yake imekuwa ya kipekee ndani ya ardhi ya Tanzania kwa msimu huu kwa wachezaji ambao wamesajiliwa dirisha dogo kwa kuwa wengi hawajaanza kuonesha makeke ikiwa ni pamoja na Thaddeo Lwanga wa Simba ambaye anatarajiwa kuanza kufanya yake Desemba 23.

Yanga, juzi (Desemba 19, 2020), waliendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Dodoma Jiji FC 3-1 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.

Kwa ushindi huo, Yanga SC ilifikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 16 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi nane zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi.

Dodoma Jiji FC yenyewe iliyopanda Ligi Kuu msimu huu inabaki na pointi zake 19 baada ya kucheza mechi 14 katika nafasi ya 11. Dodoma Jiji FC inayofundishwa na kipa wa zamani wa Yanga SC, Mbwana Makatta ilitangulia kwa bao la mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Seif Karihe dakika ya tatu tu akimalizia mpira uliotemwa na kipa Metacha Boniphace Mnata kufuatia krosi ya Dickson Ambundo kutoka upande wa kushoto.

Nahodha na beki Mghana, Lamine Moro aliisawazishia Yanga dakika ya 25 baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu na Deus Kaseke na kugeuka haraka kumtungua kipa Aaron Kalambo.

Kipindi cha pili kocha wa Yanga SC, Cedric Kaze alikianza kwa kumuingiza mchezaji mpya, Mrundi mwenzake, Said Ntibanzonkiza ambaye alikwenda kuiongezea kasi safu ya ushambuliaji na kupata mabao mawili zaidi.

Ntibanzonkiza mwenyewe aliifungia Yanga, bao la pili dakika ya 69 kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20 na ushei kufuatia yeye mwenyewe kuangushwa na kiungo Salmin Hoza nje kidogo ya boksi.
Beki mwingine wa kati, Bakari Nondo Mwamnyeto aliifungia Yanga bao la tatu dakika ya 75 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Ntibanzonkiza kutoka upande wa kulia kufutia beki KIbwana Shomari kuangushwa na Ambundo.

Mechi nyingine za Ligi Kuu juzi, Mtibwa Sugar iliichapa 1-0 JKT Tanzania bao pekee la Riphat Msuya dakika ya 43 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Ihefu iliichapa 1-0 KMC bao pekee la Joseph Kinyozi dakika ya tisa Uwanja wa Highland Estates, Mbarali mkoani Mbeya.

Nayo Gwambina ililazimishwa sare ya 1-1 na Tanznaia Prisons Uwanja wa Gwambina, Misungwi, wenyeji wakitangulia kwa bao la Paul Nonga dakika ya kwanza, kabla ya wageni kusawazisha dakika ya 81 kupitia kwa Marco Mhilu.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwanyeto, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Michael Sarpong/Said Ntibanzonkiza dk46, Deus Kaseke na Yacouba Sogne/ Ditram Nchimbi dk89.
Dodoma Jiji FC; Aaron Kalambo, George Wawa, Jukumu Kibanda, Justin Omary, Mbwana Bakari ‘Kibacha’/ Rajab Seif dk73, Salmin Hoza, Dickson Ambundo, Steven Silvester/ Cleiphace Mkandala dk84, Seif Karihe, Khamis Mcha na Peter Mapunda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here