Ni Dk. Mwinyi Zanzibar, ashinda kwa kura 380, 402

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar 

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZE), imemtangaza mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Mwinyi kuwa mshindi wa kiti hicho kwa kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote.

Akitangaza matokeo hayo leo mwenyekiti wa ZEC, Jaji Hamid Mahamoud Hamid amesema  wagombea urais walikuwa 17 waliopigiwa kura  498,786 sawa na asilimia 88.07 ya wapiga kura 566,352 waliojiandikisha.

Amesema kura zilizoharibika zilikuwa 10,944 sawa na asilimia 2.19.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 96 (2 na 3) ya Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya 2018, namtangaza rasmi Dk Hussein Ally Mwinyi wa CCM kuwa amechaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, 2020,” amesema.

Jaji Hamid amesema ZEC imehakiki matokeo ya wagombea wote wa Zanzibar na kujiridhisha kuwa yako sahihi.

Amesema mgombea anayefuatia ni Maalim Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo aliyepata kura 99,103 sawa na asilimia 19.87.

Amewataja wagombea wengine ni Said Soud Said (AAFP) aliyepata kura 285 sawa na asilimia 0.06, Juma Ally Khatib (Ada Tadea) kura 392 sawa na asilimia 0.08, Hamad Rashid Mohamed (ADC) kura 996 sawa na asilimia 0.20 na Othman Khamis (CCK) aliyepata kura 2235 sawa na asilimia 0.45.

Wengine ni Issa Mohamed (Chadema) aliyepata kura 1,702 sawa na asilimia 0.34, Ally Omar Juma (Chaumma) kura 249 sawa na asilimia 0.05, Mussa Haji Kombo (CUF) kura 1028 sawa na asilimia 2.9, Shafi Hassan Suleim (DP) kura 106 sawa na asilimia 0.02 na Amour Hassan Amour (Demokrasia Makini) kura 133 sawa na asilimia 0.03.

Mfaume Khamis Hassan (NLD) kura 122, Khamis Fakhi Mgawe (NRA) 160, Issa Mohamed Zonga (SAU) 102, Mwalimu Hussein Juma (TLP) 142, Mohamed  Omar Suleiman (UMD) kura 104 na Hamad Mohamed Ibrahim (UPDP) kura 181.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here