Ni Bunge la uwajibikaji-Spika Ndugai

0
Spika Job Ndugai

NA SHARIFA MARIRA, DODOMA

SPIKA wa Bunge Job Ndugai amewataka wabunge wa Bunge la 12 kufanya kazi yao ya kikatiba ya kuisimamia serikali na kutokuwa mabubu kwani kufanya hivyo tutakuwa kunawaharibia wenyewe kwa wananchi wao waliowapa dhamana.

Aidha bunge hilo hakutakuwa na kambi rasmi ya upinzani kwasababu haijafikia asilimia 12.5 ambayo ipo kwa mujibu wa sheria.

Ndugai alisema licha ya kuwa  idadi kubwa ya wabunge ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) litasimamia ipasavyo majukumu ya kuisimamia na kuishauri serikali kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

Alitoa kauli hiyo jana baada ya kula kiapo cha kuongoza bunge hilo ikiwa ni mara ya pili kupata wadhifa wa kuongoza muhimili huo kwa kura za ndio 344 huku kura ya hapana ikiwa moja kati ya kura 345 zilizopigwa na wabunge ikiwa ni sawa na asilimia 99.7.

“Bunge hili litakuwa la uwajibikaji na hakuna kubebana. Kama ukichagua kuwa mbunge bubu, husemi, upo upo tu ili uonekane una nidhamu kwenye chama, huku umejimaliza mwenyewe.

Alisema “Kunyamaza sio nidhamu, wananchi wamekuchagua uwasemee, watafurahi kama fikra na mawazo yao yanawasilishwa ipasavyo.

Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM), alisema licha ya idadi kubwa ya wabunge ni kutoka CCM, chombo hicho kitatekeleza wajibu wake ipasavyo, hivyo wabunge watakaochaguliwa kuwa mawaziri na manaibu mawaziri, wanapaswa kuwajibika na hakuna kubebana.

Aliwapongeza wabunge kwa kuchaguliwa kuwakilisha wananchi kutokana na heshima na matarajio makubwa waliyokuwa nayo wananchi kwa viongozi hao.

“Mnapaswa kuhakikisha hamtoangusha matarajio ya wananchi, mnapaswa kutunga sheria, kuisimamia na kuishauri serikali pamoja na rasilimali za nchi. Kazi haitokuwa nyepesi, Bunge hili linapaswa kutoa matokeo chanya,” alibainisha.

Pia aliwataka wabunge kusoma kanuni za Bunge ili kufahamu masuala muhimu yanayohusu Bunge katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwemo taratibu za mavazi.

Vilevile, aliwataka wabunge kujiepusha na tabia ya kukopeshana fedha ambapo alisema Bunge lililopita kuliibuka changamoto ya aina hiyo, hivyo endapo wabunge wakikopeshana ofisi yake haitohusika.

Spika Ndugai aliwatoa hofu wabunge kutoka vyama vya upinzani ambapo aliwaeleza katika bunge hilo haki zao za msingi zitazingatiwa.

MCHAKATO WA UCHAGUZI

Awali Katibu wa Bunge, Stevin Kagaigai, aliongoza kikao cha bunge ambacho kilianza na ratiba ya uchaguzi kwa kumchagua Spika wa bunge ambapo wabunge walimteua mwenyekiti wa muda, ambaye ni mbunge aliyedumu bungeni kwa muda mrefu, Mbunge wa Isimani (CCM) William Lukuvi, kuendesha kikao hicho.

Kagaigai alianza kwa kusoma tangazo la rais kuitisha Bunge na tangazo la kuvitaka vyama vya siasa kuwasilisha majina ya wagombea kwa nafasi ya kiti cha Spika wa Bunge.

“Kufuatia tangazo la Rais kuitisha bunge lililotangazwa kwenye Gazeti la Serikali, toleo maalum la Novemba 5, 2020 (Tangazo No 942A), na kufuatia tangazo nililolitoa kwenye Gazeti la Serikali, Toleo Maalum la Novemba 5, 2020 (Tangazo Namba 1763A) kuhusu nafasi ya Spika kuwa wazi na utaratibu utakaotumika kujaza nafasi hiyo pamoja na Gazeti la Serikali toleo maalum (Tangazo Namba 1764A),” Katibu huyo wa Bunge, alisema.

Mara baada ya kusoma tangazo hilo, alisema mpaka kufika Novemba tisa mwaka huu ambayo ndiyo ilikuwa siku rasmi ya wagombea kuwasilisha majina kupitia vyama vyao, hadi saa 10 jioni alikuwa amepokea jina la mgombea mmoja kutoka CCM ambaye ni Ndugai.

“Shughuli hii ya uchaguzi tunaifanya kwa mujibu wa Ibara ya 84, kifungu kidogo cha kwanza kikisomwa pamoja na Ibara ya 68 ya katiba,” alisema katibu.

Katibu huyo wa Bunge alifafanua kuwa ilipofika saa 12 jioni, alipokea barua pepe ya mgombea kutoka Chama cha NLD, Bonaventura Ndekeja, akiomba kuwania nafasi hiyo.

Alisema mgombea huyo hakukidhi vigezo kutokana na kuchelewa kuwasilisha maombi yake ambapo alipeleka barua hiyo ikiwa muda wa kurejesha fomu ulishafikia mwisho.

“Pia mgombea anayeomba kugombea kiti cha Spika kwa mujibu wa kanuni akiwa si mbunge chama chake kinapaswa kupeleka jina hilo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ili liweza kuthibitisha kama mgombea huyo anazo sifa za kugombea, lakini hilo halikufanyika hivyo kumfanya mgombea kupoteza sifa,” alieleza.

Katibu huyo alisema wabunge waliokuwa ndani ya ukumbi kwa wakati wa kupiga kura walikuwa 263 hivyo kufanya akidi ya wapiga kura kuwa imetimia.

“Wabunge watapiga kura za ndio au hapana na kura hizo zitakuwa za siri na kama mbunge ataharibu karatasi ya kupigia kura, anyoshe mkono ili katibu aichukue na kumpatia nyingine,” alisema Kagaigai.

Akiendesha uchaguzi huo Lukuvi, alisema kazi iliyoko mbele yao muhimu hivyo lazima waikamilishe kwa sababu hakuna mbunge anayeweza kuapa pasipo kuwepo kwa spika.

Baada ya wabunge kupiga kuwa, saa 4: 29, msimamizi wa uchaguzi huo, Lukuvi alimtaka Katibu wa Bunge kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Kagaigai alisema wakati wa uchaguzi idadi ya wabunge ilifikia 345 kutoka 263 ya awali na kufanya idadi ya wabunge waliopiga kura kuwa 345.

Ndugai anashika wadhifa huo kwa mara ya pili ambapo katika Bunge la 11, alichaguliwa kwa kura 254 huku aliyekuwa mpinzani wake Goodluck Ole Medeye, kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alipata kura 109.

Job Ndugai, akiapa kuwa Spika wa Bunge baada ya kuchaguliwa kwa kura 344 kati ya kura 345 zilizopigwa ushindi ambao ni sawa na asilimia 99.7.

MAONI YA WABUNGE

Mbunge wa Nzega Vijijini (CCM) Dk. Hamisi Kigwangala, alisema kuchaguliwa kwa Ndugai anatarajia kuendelezwa kwa utendaji uliotukuka, mzuri kutokana na usikivu wake, unyenyekevu na uweredi.

“Naamini ataliongoza bunge hili kwa kuzingatia vigezo vyote, kama ambavyo ameweza kufanya katika vipindi vilivyopita tangu alivyokuwa Naibu na Spika wa Bunge. Yeye anakipindi cha pili, ana uzoefu, ninamfahamu, nina muamini kutokana na utendaji wake, atalitendea haki Bunge la 12,” alisisitiza.

Mbunge wa Nanyamba ,Abdallah Chikota,alisema mbunge ana dhamana kwa wananchi, kwa chama na uwakilishi wake kwahiyo mtu akiamua kuwa bubu wale ambao uliwaomba kura watajua kuwa husemi kitu kwa maana hiyo hutaki kusimamia ilani hivyo hawatakuamini tena kwahiyo unakuwa unajitengeneza madiba mwenyewe.

“Bunge hili asilimia kubwa ni CCM kazi kubwa ni kusimamia serikali tutajitahidi kutoa mawazo ya kujenga na chama hakizuii mtu yeyote kutoa mawazo yake ya kujenga kwa serikali isipokuwa tusiwe tunapinga kila kitu “

Akizungumzia maoni kuhusu Bunge la 12, Mbunge wa Singida Mjini (CCM) Mussa Sima, alisema katika bunge hilo atazingatia ushauri wa spika wa kutokaa kimya kwani atahakikisha changamoto za wananchi anazieleza kwa kina.

Mbunge wa Kwaani (CCM), Ahmed Yahya Abdulwakil, alisema Spika ametoa wosia wenye uzito kwa wabunge wa CCM kutumia wingi wao kueleza changamoto za wananchi kwa kuwasemea maoni yao.

Mbunge wa Buchosa, Erick Shigongo, alisema “Mimi naamini kwenye watu wenye uhuru wa mawazo siwezi kuwa nasema tu kwasababu spika amesema na sitegemei kunyamaza sehemu ambayo natakiwa kuongea,”

Lakini pia “siwezi kuongea kwasababu natafuta sifa ili nionekane muongeaji, nitakuwa naongea kwa hoja pale inapohitajika nitakuwa mwakilishi mzuri sitawaangusha walionichagua,nafsi yangu itakuwa inanisuta kwani nimetoka katika familia masikini na watu wangu ni masikini sasa nisipowasemea nitakuwa nawakosea”

Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei, alisema kutokana na kuwa asilimia kubwa ya wabunge wa  bunge hilo ni kutoka chama kimoja kuna wengine wataona kwamba hakuna haja ya kuishauri serikali jambo ambalo ni kosa, serikali inapaswa kusimamiwa na bunge  na wabunge ndio kazi yao.

“Baadhi ya watu wanaweza wakaona kwamba hakuna haja ya kuchangia kwasababu bunge lina wabunge wa chama kimoja lakini katika kipindi ambacho bunge linaweza kuisaidia serikali ndio hiki ni vyema kuchangia kitu ambacho kinaenda kujenga uchumi,kinaenda kuongeza ajira, kuchangia vitu ambavyo ni “constructive” alisema na kuongeza kuwa

“Ni vyema watu wajiamini na kujenga hoja ambazo zitajenga na kuivusha nchi yetu kiuchumi, kukaa kimya ni kuwakosea wananchi waliokupa dhamana lakini pia kujikosea wewe mwenyewe kwani  utakuwa unalipwa bila kufanya kazi jambo ambalo ni dhambi “

Naye Mbunge wa Rombo,Profesa Adolf Mkenda, alisema  kuwa mbunge wa CCM hakumuondolei  mtu yeyote wajibu wake wa kikatiba wa  kuisimamia na kuishauri serikali isipokuwa ni namna gani mtu anashauri au anasimamia ndio kinazingatiwa.

“Bunge hili mimi naamini tutafanya kazi kubwa sana maana naona tutaishauri serikali kwa hoja, tutawasemea wananchi cha muhimu tukosoe kwa kweli kwa uwazi kwa nia ya kujenga, sio hata sehemu ambayo tunajua serikali imefanya vizuri tupinge tu tutakuwa hatufanyi kitu “alisema Profesa Mkenda

Mbunge wa Arusha Mjini ,Mrisho Gambo,alisema “Sitawacha wananchi walionichagua,nitafanya kazi yangu kikatiba,sitakuwa mbunge bubu,nitasema shida na kero za watu na kuwasemea na  hiyo ndio itakuwa salama yangu kwani nisipofanya hivyo baada ya miaka mitano sitakuwa na cha kuwaambia,”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here