Ni Bunge la kazi tu

0

NA DOTTO KWILASA,DODOMA

Ndivyo unavyoweza kusema wakati Mkutano wa kwanza wa Bunge  la 12 la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, unatarajiwa kuanza leo Jijini hapa ambapo Wabunge wateule  wanatarajiwa kuanza kula viapo vya kiwatumikia Wananchi.

Tofauti na Bunge lililopita Bunge la sasa limesheheni wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioshinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Bunge,Dk.Steven  Kagaigai ilieleza kuwa wabunge wateule kila mmoja anapaswa  kuambatana na wageni wasiozidi 20 wakati wa zoezi la kuapa linalotarajiwa kuanza leo hadi keshokutwa. (Novemba 10 hadi 12) ambapo  zoezi hilo litafanyika  kwa muda mfupi.

HALI ILIVYO

Wabunge wengi wateule wameishafika Jijini hapa wakiwa na wapambe pamoja na baadhi ya ndugu kwa ajili ya kuapishwa zoezi ambalo litadumu kwa siku mbili.

Wabunge wengi wamekuwa wakihaha kupata nyumba ambapo baadhi ya madalali wa nyumba wamesema kwamba siku hizi mbili zimekuwa za neema kwao.

Baadhi ya madalali hao walisema maeneo ambayo Wabunge hao wateule wamekuwa wakitaka nyumba ni Area C,Area D,Kisasa,Uzunguni pamoja na Swaswa.

Mabutu Seseko alisema baadhi wamepata lakini wengine wamekuwa wasumbufu kwani kila nyumba anazopelekwa wamekuwa wakizikataa kwa kudai hazina hadhi zao.

“Ila kuna Wabunge wale wa zamani wengi wamejenga lakini hawataki kuwapangisha Wabunge wenzao sijui ni kwanini,ila hawa wageni wanataka kwa wingi na sisi tumekuwa tukipata fedha kwani kumuonesha tu nyumba 20,000 akikataa nyumba ananipa change tunaendelea kutafuta kwingine,”alisema.

Katikati ya Jiji la Dodoma migahawa maarufu ya Chief Asili,Emirates,Mwambao ilikuwa na watu wengi huku baadhi ya wabunge wateule wakiuonekana na ndugu zao pamoja na wapambe.

Katika ‘Internet Cafe’ baadhi ya Wabunge hao walionekana wakijaza baadhi ya ‘document’ ambazo wanatakiwa kuzipeleka bungeni kama ambavyo waliagizwa na Ofisi ya Bunge ikiwemo kutoka ‘photocopy’ vyeti vya elimu,

Waosha magari jirani na Ofisi za Bunge wakizungumza nao walidai kwamba ujio wa Wabunge wapya ni faraja kwao kwani watajipatia kipato kwa kuosha magari yao.

Juma Isack alisema wakati wa Bunge hugeuka kipindi cha neema kwao hivyo anaimani kipindi hichi itakuwa neema zaidi kwani wabunge wapya na wale wa zamani watataka kuosha magari yao.

“Wakipark tu hapa naimani watataka kuosha magari yao na sisi tutajipatia kipato,”alisema.

WABUNGE WATEULE WAOMBA USHIRIKIANO.

Wakizungumza  nje ya viwanja vya Bunge mara baada ya kujiandikisha,baadhi ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliomba ushirikiano kwa wananchi waliowachagua huku wakiahidi kuwasemea katika Bunge hilo kuhusiana na matatizo ambayo yapo katika Majimbo yao.

MAKOA NA USHIRIKIANO

Mbunge  mteule wa Jimbo la Kondoa Mjini,Ally Makao alisema katika kipindi cha miaka mitano atajitahidi kuboresha maisha ya wana Kondoa ikiwa ni pamoja na kusimamia shughuli za maendeleo huku akiomba ushirikiano kwa wananchi.

“Nawashukuru Wananchi  wa Jimbo la Kondoa kwa kunichagua kikubwa naendelea kuwaomba ushirikiano ili tuweze kuchapa kazi yenye kuonekana watu wa Kondoa wanapaswa kujiandaa kufanya kazi kwa pamoja na tutaungana kwa pamoja kufanya kazi.

“Kondoa ni sehemu nzuri yenye ardhi ya kutosha na rutuba kuna mito ambayo inaweza kutumika katika kilimo,tuna uwezo wa kufuga.Katika kipindi changu cha miaka mitano tutajikita zaidi kuboresha maisha ya wanakondoa,”alisema.

MBUNGE ZEDI NA UMEME

Kwa upande wa Mbunge Mteule wa Bukene,Seleman Zedi alisema kuna mambo mengi ya       kuanza nayo katika Jimbo lake ikiwemo kuhakikisha vijiji ambavyo bado havijapata umeme vinapata pamoja na maji.

“Wananchi wa Jimbo langu kuna mambo mengi ambayo tumeyaanza yalikuwa hajafika mwisho la kwanza watarajie yale mambo ambayo yapo katikati sasa ndio tunaanza na umeme,maji.Ule mradi wa Bomba la mafuta unapita kwangu hivyo hili nalo tutafanya nalo na mambo mengine pia tutayafanyia kazi,”alisema.

DK CHAYA NA MANYONI YAKE 

 Mbunge mteule  wa Manyoni Mashariki,Dk.Pius Chaya alisema yeye ni Mbunge mpya hivyo anaimani Mwenyezimungu atamsaidia na ataweza kuwasemea watu wa Manyoni ambao wana shida nyingi ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi.

ASKOFU GWAJIMA NA BARABARA

Kwa upande wake,Mbunge Mteule wa Kawe, Askofu osephat Gwajima alisema kipaumbele chake cha kwanza ni barabara za ndani na maji.

“Ninafuraha kuhudhuria Bunge hili la 12 hasa kuingia katika mkutano wa kwanza wa Bunge hili na nipo hapa kwa sababu ya Wananchi wa Kawe nataka kila linalowezekana maisha yao yawe mazuri.Kipaumbele changu cha kwanza ni  barabara zote za ndani hazipo vizuri ni mbovu   Magwepande Bunju Mikocheni kote kule barabara hazipo vizuri.

Alisema kipaumbele chake kingine ni upatikanaji wa maji kwani baadhi ya maeneo upatikanaji wake haupo vizuri.

TARIMBA NA UBUNGE KUWA TAASISI

Naye,Mbunge Mteule wa Kinondoni Tarimba Abassi alisema  anataka kuwa mtumishi wa kweli kwa waannchi kwa kuwatumikia wakati wowote ambapo alidai kwamba ataufanya Ubunge wake kuwa ni Taasisi ambayo wananchi wataifikia wakati wowote hata kama yeye atakuwa hayupo.

“Kwanza nataka niwe mtumishi wao wa kweli nataka kuleta mabadiliko siwasemi vibaya Wabunge waliopita mimi nitataka  nilete mabadilo kwa kuwa karibu.Naifahamu Kinondoni vizuri Ubunge wangu nitaufanya uwe ni Taasisi kutakuwa na Maafisa wangu ambao watakuwa wakiwatumikia wananchi kwa niaba yangu,”alisema Tarimba.

DK.NDUGULILE NA AHADI

Mbunge Mteule  wa Kigamboni,Dk.Faustian Ndugulile aliwaahidi waakzi wa Kigamboni kwamba yale yote aliyaahidi waklati wa kampeni atajitahidi kuweza kuyatimiza.

“Nataka niwaambie wana Kigamboni Mbunge wao nimefika Dodoma na niwaahidi yale yote niliyosema wakati wa kampeni tutayafanyia kazi kuleta maendeleo,”alisema.

SHUGHULI ZITAKAZOFANYIKA 

Akizungumza na Waandishi wa Habari wiki iliyopita,Katibu wa Bunge,alisema shughuli zitakazofanyika katika mkutano huo wa kwanza wa Bunge la 12  ni pamoja kusomwa tangazo la Rais la kuitisha Bunge,uchaguzi wa Spika,kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote,kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu na uchaguzi wa Naibu Spika.

RAIS KUFUNGUA BUNGE

Aidha Katibu huyo wa Bunge alisema shughuli nyingine itakayofanyika wakati wa mkutano huo ni ufunguaji rasmi wa Bunge jipya utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk.John Magufuli.

Alipoulizwa na Waandishi wa Habari siku ya kwanza ya ufunguzi wa Bunge ndipo  Rais atalifungua na kulihutubia  Bunge hilo ama ? Dk.Kagaigai alisema: “ Hapana  siku ya Rais kuja kulifungua Bunge tutatoa taarifa,”.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here