NEC yavitaka vyama vya siasa kuwasilisha Orodha ya mawakala kesho

0

MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa kuwasilisha orodha na barua za utambulisho wa mawakala wao kwa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo husika kesho Jumatano  Oktoba 21, 2020.

Kauli hiyo imekuja ikiwa zimebaki siku saba kufikia Oktoba 28, 2020 siku ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Oktoba 20, 2020  na mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Kaijage amesema utaratibu huo wa kuteua mawakala, kuwaapisha, kuwapangia vituo na utambulisho wao kwa wasimamizi wa vituo umeanishwa chini ya kifungu cha 57 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na kifungu cha 58 cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vikisomwa pamoja na kanuni za 50 na 43 zilizotungwa chini ya sheria hizo.

Amesema utaratibu huo wa kisheria pia umefafanuliwa katika vijitabu vya maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea na maelekezo kwa mawakala wa vyama vya siasa na wagombea vya mwaka 2020 ambavyo tayari NEC  imevipatia vyama vya siasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here