Ndayiragije, Kaseja wafunguka kuelekea mechi na Tunisia

0

NA MWANDISHI WETU

MMOJA kati ya wachezaji wazoefu katika timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ mlinda mlango, Juma Kaseja, amesema mchezo wao dhidi ya Tunisia utakuwa mgumu kwa sababu wanacheza ugenini na wanahitaji matokeo mazuri.

Ikumbukwe Kikosi cha Taifa Stars kiko mjini Istanbul,Uturuki ambako kimeweka kambi ya siku tano kabla ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2021), dhidi ya Tunisia Novemba 13.

Mchezo huo, wa kundi J utachezwa mjini Tunis, huku Stars ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita wa kundi hilo kwa kufungwa na Libya mabao mawili kwa moja, huku ikishinka nafasi ya tatu kwa kufikisha alama tatu.

Stars iliifunga Equatorial Guinea mabao mawili kwa moja, kwenye mchezo wa kwanza wa kundi hilo uliochezwa Dar es salaam Novemba mwaka 2019.

Kaseja, alisema ugumu huo unatokana kutokana na wapinzani wao kuwa na maadalizi yao dhidi ya mchzo huo huku akisisitiza kuwa hata wao wamejiandaa.

“Mechi itakuwa ni ngumu kwa sababu tunacheza ugenini na wao wana mipango yao ya mchezo huo, ambayo wamejiandaa lakini na sisi vilevile mwalimu ameandaa mindunu za kwenda kucheza nao kwa hiyo mchezo hauwezi kuwa rahisi.

“Mchezo utakuwa mgumu lakini yote kwa yote naamini kikubwa ni kujiandaa kwa sababu hakuna jinsi tutakutana wao 11 na sisi 11 ndani ya uwanja kwa wale watakao kuwa vizuri watapata matokeo.

“Timu inamaeneo mengi viongozi wa Shirikisho wamejitahidi kutoa timu Dar es Salaam kuileta Uturuki kwa maandalizi lakini lakini yote kwa yote ni maandalizi kwa ajli ya mchezo huo kwa hiyo wao kama wao wameishatimiza wajibu wao, wajibu uliobaki ni kwa wachezaji kwenda kupambana kuhakikisha tunapata alama tatu,”alisema Kaseja

Kaseja, alisema lengo la kila Mtanzania ni kuona timu inapata alama tatu, kama hawakupata alama tatu basi wapate japo alama moja kwa maana yakutoka sare kwa sababu bado wana michezo mingine.

“Wao naamini watataka kuja kumaliza mchezo katika dakika 10 hadi 20 za kwanza kwa hiyo, hivyo ni vitu ambavyo mwalimu kaongea naamini kila mchezaji atatakiwa aweke akilini kuhakikisha ndani ya dakika 10, 20 za kwanza umakini uwe kwenye hali ya juu ili kuzuia hilo lisitokee.

“Naamini zikipita ndani ya dakika 20 hawajapata goli basi mchezo utapoa lakini naamini mchezo utakuwa mgumu kwa sababu wao wanahitaji matokeo katika mchezo huo ili kujihakikishia nafasi nzuri.

“Lakini hata sisi tunahitaji matokeo ili kujihakikishia nafasi kwa sababu tuna michezo mingine miwili nyumbani kwa hiyo tunaamini kama kila mmoja atatekeleza yale mwalimu anaelekeza basi gemu inaweza kuwa nzuri kwa upande wetu kwa sababu kuna vijana wengi wenye uwezo na si mara ya kwanza kucheza mechi kama hizi zenye mhemko,”alisema Kaseja.

Juzi Kocha Mkuu wa Stars Ettiene Ndayiragije, alisema kikosi chake kipo tayari kwa maandalizi ya siku kadhaa nchini Uturuki, na ana matumaini makubwa ya kufanya vyema mbele ya Tunisia ambao wanaongoza msimamo wa kundi ‘J’, kwa kufikisha alama 6.

Alisema, aliwafuatilia Tunisia na kubaini mbinu zao wanapokua uwanjani, hivyo atatumia siku hizo tano za maandalizi kuwaandaa vyema wachezaji wake ambao wanaonekana kuwa na ari kubwa ya kupambana.

Ndayiragije, alisema alianza maandalizi ya mchezo huo muda mrefu, kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na wachezaji aliowaita na kuwaeleza umuhimu wa kupambana ili kupata matokeo.

“Nimewafuatilia wapinzani wetu, hivyo tutawakabili tukiwa tunawafahamu ubora na udhaifu wao,”alisema kocha huyo kutoka nchini Burundi.

Wachezaji walioitwa Taifa Stars kwa ajili ya mchezo huo ni Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Adam Adam, Juma Kaseja, Metacha Mnata, Aishi Manula, David Mapigano, Shomary Kapombe, Deus Kaseke, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Brayson David na Bakari Mwamnyeto

Wengine ni  Abdallah Kheri, Jonas Mkude, Himid Mao, Erasto Nyoni, Simon Msuva, Ditram Nchimbi, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Ally Msengi, John Bocco, Mzamiru Yassin, Iddy Suleiman, Thomas Ulimwengu, Farid Mussa, Said Mussa, Said Ndemla, Salum Abubakar, Adam Adam na nahodha Mbwana Samatta.

Hata hivyo, Nahodha wa Taifa Stars Samatta, hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachovaana na timu ya Taifa ya Tunisia Novemba 13.

Samatta ambaye ni mshambuliaji jina lake lilitajwa katika orodha ya wachezaji 27 walioitwa kuunda kikosi cha Timu ya Tanzania.

Kwa sasa Stars chini ya Kocha Mkuu, Ndayiragije imeweka kambi nchini Uturuki ambapo nyota huyo anacheza nchini humo.

Habari zinaeleza kuwa Samatta hayupo kwenye mazoezi na timu ya Taifa ya Tanzania kwa kuwa ana matatizo ya kiafya na ameshauriwa na madaktari kutocheza ili arejee kwenye ubora wake.

Taifa Stars inatarajiwa kuondoka nchini Uturuki kuelekea Tunisia leo kwa ajili ya mchezo huo Siku ya Ijumaa Novemba 13 mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here