Nataka TRC iwe mfano Afrika: Magufuli

0

Rais Dk. John Magufuli amesema anataka kulifufua Shirika La Reli Tanzania ili liwe mfano kwa nchi zingine barani Afrika zinazotumia usafiri kama huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa safari za treli Dar es Salaam-Arusha Rais Dk.  John Magufuli alisema kulifanyika makosa makubwa kwa kubinafsisha sekta nyeti za usafiri ikiwemo reli, ndege na meli hivyo iwe fundisho kwa viongozi wengine.

Mikoa ya kanda ya Kaskazini inakwenda kuimarika kwa miundombinu ya usafiri baada ya kufufuliwa rasmi usafiri wa treni kati ya Dar es Salaam, Tanga hadi Arusha uliosimama kwa zaidi ya miaka 30.

Aliweka wazi kuwa kwa sasa wana mpango wa kununua vichwa vya Treni 39 kwa njia kuu, Vichwa 18 vya Sogeza Sogeza, Mabehewa 800 ya mizigo na 37 ya abiria.

“Tunataka shirika hili liwe mfano kwa Afrika kwa mashirika yanayofanya Biashara na kazi kwa kuhudumia wananchi wake wakiwemo wanyonge.

“Treni hii tukaanza upya tulikuwa na Meli zilizoachwa tangu enzi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere zikabinafsishwa naomba suala hilo liwe fundisho,” alisema.

Alibainisha, yeye hatokuwa  rais  wa maisha hivyo anatoa fundisho kwa viongozi watakaokuja baadae  ili iwe fundisho kwao kutorudia kubinafsisha vitu hivyo.

“Tulipobinafsisha Shirika la Reli wakawa wanachukua mabehewa yetu wanapeleka kule, kwa hiyo hapakuwa na chochote, watendaji nao wakastaafishwa na wafanyakazi wakaachishwa  kazi hili tunajifunza .

“Ndio maana niliwaambia watendaji wa TRC kwamba ni lazima tufanye mabadiliko tuachane na yule Mbia tujipange sisi watanzania kupanga mambo yanayotuhusu,” alisema.

Aliwashukuru watendaji wa Shirika hilo la reli nchini kwa kufanya maajabu kwaajili ya taifa kwani kuna wakati walimfata na kumuomba kiasi cha fedha Sh Bilioni 5 kwa ajili ya kufufua mabehewa.

Alifafanua, kwa kuwa watendaji hao wamefanya makubwa Wizara ya Uchukuzi itaendelea kuwaunga  mkono mara watakapomaliza uchaguzi mkuu.

TRC hakikisheni mnaimarisha na kuboresha huduma zenu na kuhakikisha gharama zinakuwa chini pia kuweni mstari wa mbele kupinga rushwa ili watanzania wanufaike na usafiri huu,”alisema.

Pia, aliwataka watanzania hususani wakazi wa mikoa ya Kaskazini kutumia reli hiyo vizuri ili wanufaike nayo kwani ni wajibu wao kulinda miundombinu hiyo.

“Kuna wakati palikuwepo na  watu waliokuwa wanafanya njama kuharibu reli naomba watanzania wa kanda hii na mahali popote panapopita treni watunze ili iweze kutuhudumia vizuri, ujio wa treni hili utasaidia uchumi wake kupanda na watu kufanya biashara,’’ alisema.

Dk. Magufuli aliongeza kuwa kwa sasa TRC wameongeza abiria kwenye reli ya Dar es Salaam kutoka milioni 1.27 kwa mwaka 2014/15 hadi abiria milioni 6.73.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here