Mwanamfalme William alikutwa na maambukizi ya covid-19

0

LONDON,UINGEREZA 

MWANAMFALME William alikutwa na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 mwanzoni mwa mwaka huu, vyanzo vimeiambia BBC.

Inaaminika kuwa alikutwa na maambukizi ya virusi vya corona mwezi Aprili wakati huo huo, baba yake mwanamflame wa Wales alipokutwa na maambukizi.

Kwa mujibu wa gazeti la the Sun, ambalo liliripoti kwanza taarifa hiyo, mwana mfalme William, 38, aliifanya taarifa hiyo siri kuepuka kuliweka taifa katika taharuki.

Kasri la Kensington, ofisi na makazi ya mwanamfalme William, ilikataa kutoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo.

Mwanamfalme William, hakumwambia mtu yeyote kuhusu majibu ya vipimo kuwa na maambukizi kwasababu ”kulikuwa na masuala muhimu yaliyokuwa yakiendelea na sikutaka kusababisha hofu”, kwa mujibu wa the Sun.

Alitibiwa na madaktari wa kasri, alifuata ushauri wa serikali kwa kujitenga katika makazi ya familia Anmer Hall, huko Norfolk, gazeti hilo liliongeza.

Mwandishi wa habari za kifalme, Jonny Dymond, alisema kuwa hali ya mwanamfalme William haikuwekwa hadharani ili kuepusha taharuki zaidi wakati huo.

”Lakini kasri la kifalme limejaribu kutunza siri za familia hiyo,” alieleza mwanahabari huyo.

Mwanamfalme William aliripotiwa kufanya mazungumzo ya simu 14 na video kipindi cha mwezi Aprili.

Awali mwezi huo, Mwanamfalme na mkewe waliwapigia simu ya video watoto wa wafanyakazi muhimu katika shule ya msingi mjini Lancashire.

Prince Charles alikutwa na maambukizi ya virusi vya corona mwezi Machi na kujitenga kwa siku saba huko Scotland baada ya kuonesha dalili za wastani.

Mwezi Aprili , Boris Johnson alilazwa hospitalini baada ya kukutwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Waziri Mkuu alihamishiwa kwenye chumba cha wagonjwa walio chini ya uangalizi maalum na baadae aliwashukuru wahudumu wa afya kwa kuokoa maisha yake.

Taarifa za Prince William zimekuja siku chache kabla ya Uingereza kuingia kwenye awamu ya pili ya sharti la kutotoka nje, hatua itakayochukua majuma manne kuanzia Alhamisi.

Watu 23,254 walithibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona siku ya Jumapili, na kufanya idadi kufikia 1,034,914 tangu kuanza kwa janga hilo.

Watu wengine 162 waliripotiwa kupoteza maisha ndani ya saa 28 na kufanya idadi ya waliofariki kutokana na ugonjwa huo kufikia 46,717

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here