Mwambe:Bei ya mafuta itatengemaa tukimaliza upakuaji

0

NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM

WIKI hii baadhi ya   vyombo mbalimbali vya habari  nchini  wameripoti kuhusu uhaba wa mafuta ya kula ambapo wengi wao walidai yamepanda katika bei za juu jambo linalosababisha wananchi wa kawaida kununua bidhaa hiyo kwa bei ya juu.

Bidhaa hiyo ambayo ni muhimu hasa kwa wafanyabiashara   mbalimbali ikiwemo  vyakula  taarifa ya kuadimika kwake  kumedai kuleta taharuki na kusababisha bei kupanda.

Jana  Waziri wa Viwanda na Biashara Geoffrey Mwambe amewahakikishia wananchi kuwa hali ya upatikanaji wa mafuta ya kula itatengemaa mara baada ya kuanza upakuaji wa mafuta ya kula yanayoingizwa kutoka nje ya nchi kupitia bandari yetu ya Dar es salaam.

Amesema changamoto ya uhaba wa mafuta ya kula umetokana na upungufu wa uzalishaji na kutegemea uagizaji wa mafuta ya kula nje ya nchi, bei ya mafuta ya kula hutegemea soko la bidhaa hiyo kulingana na msimu na mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo katika soko la Dunia.

“Serikali imezipatia leseni kampuni mbili za uagizaji wa mafuta ya kula ambazo ni East Coast Oil and Fats Ltd na Murzah Wilmar East Africa Ltd. Kampuni hizo zimekuwa zikiingiza mafuta ya kula nchini ili kukidhi upungufu wa tani 365,000 MT kwa mwaka ya mahitaji halisi ya mafuta hayo ya tani 570,000 MT kwa mwaka wakati kiasi kinachozalishwa nchini ni tani 205,000 MT kwa mwaka (TARI-2020),”amesema Mwambe.

Amesema pia  meli mbili zimeingia bandari ya Dar es salaam. Meli aina ya UACC SHMIYA iliyowasili Bandari ya Dar es Salaam tarehe 10 Desemba, 2020 ambayo ilipangwa kushusha shehena tarehe 11 Januari, 2021, iliruhusiwa kuanza kushusha shehena husika kuanzia tarehe 30 Desemba, 2020 na kukamilisha ushushaji tarehe 03 Januari, 2021.

“Kiasi cha mafuta ya kula yenye ujazo wa 21,800 MT kimepakuliwa katika meli hiyo na sasa kiko tayari kuingia sokoni.  Aidha, meli nyingine iitwayo MELATI SATU ya shehena ya mafuta ya kula ya ujazo wa 26,450 MT imetia nanga alfajiri ya tarehe 5 Januari, 2021 katika Bandari ya Dar es Salaam na ratiba ya ushushaji wa shehena inaonesha kuwa ni tarehe 19 Januari, 2021 hadi tarehe 22 Januari, 2021.

“Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inaharakisha ushushaji wa mafuta ya kula yanayoingia kutoka nje ya nchi kupitia bandari ya Dar es salaam ili kuharakisha upatikanaji wa mafuta kwa wananchi na kupunguza kupanda kwa bei,”amesema Mwambe.

Pamoja na hayo Wizara imewekeza nguvu katika mkoa wa Kigoma kupitia agizo la Waziri Mkuu kuhusu ushiriki wa Taasisi za Umma katika uzalishaji wa mchikichi kwa ajili ya usindikaji wa mafuta ya kula.

Amesema taasisi hizi ni pamoja na Jeshi la Magereza Tanzania, Taasisi ya utafiti wa Kilimo (TARI), na Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo na Biashara ndogo (SIDO).

“Vilevile, Serikali imeendelea kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vikubwa, vya kati na viwanda vidogo vya kusindika mbegu za mafuta ili kutatua tatizo la uhaba wa mafuta ya kula nchini,”amesema Mwambe.

Tamko la Mwambe limekuja baada ya gazeti moja la kila siku kuripoti kuwa  bei ya mafuta ya kula sasa haikamatiki katika maeneo mbalimbali nchini huku pia bidhaa hiyo muhimu ikianza kuadimika.

Kutokana na bei kupanda baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wamei sasa wanatumia mafuta mbadala, hasa ya wanyama kama vile kondoo, kwa ajili ya kupikia.

Gazeti hilo lililofanya  katika mikoa tofauti nchini na kubaini kupanda kwa bei ya mafuta ya kula ya alizeti na yale yanayoagizwa kutoka nje, yote yakiuzwa kwa bei mbayo haikuzoeleka.

Kupanda kwa bei ya mafuta ya kula, kumesababisha kupanda kwa bei ya vyakula vilivyoandaliwa kama vile chips na vitafunwa mbalimbali.

Serikali imekiri kuwepo kwa uhaba wa mafuta nchini ambayo inaelekea kwisha baada ya kuwasili kwa meli za mafuta.

Mwenyekiti wa chama cha wasindikaji wa mafuta ya kupikia Tanzania (Tasupa), Ringo Iringo alitaja sababu mbili zilizosababisha bei ya mafuta kuwa juu nchini.

Iringo amesema mvua kubwa zilizonyesha katika msimu wa mwaka jana ni moja ya sababu kwa kuwa mavuno yalikuwa kidogo katika msimu huo na kufanya wenye mafuta wayapandishe bei.

Amesema zao la alizeti ambalo ndilo linazalisha mafuta kwa wingi halihitaji mvua kubwa lakini katika msimu wa mwaka jana mvua zilinyesha kwa wingi kiasi cha kuharibu mazao hayo mashambani.

Mwenyekiti huyo alisema katika maeneo mengi ambako wanategemea kilimo cha alizeti, wengi hawakuvuna ama walivuna chini ya wastani, hivyo, kusababisha bidhaa hiyo kuwa adimu na viwanda vingi kusimamisha uzalishaji wa mafuta.

“Lakini sababu nyingine ni sheria iliyopitishwa bungeni ambayo iliongeza ushuru wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje na kuwafanya wafanyabiashara wengi kuachana na biashara hiyo na kupelekea mahitaji ya mafuta kutegemea zaidi uzalishaji wa ndani,” amesema Iringo.

Mwenyekiti huyo alisema mahitaji ya mafuta nchini ni tani 570,000 wakati kiasi kinachozalishwa ni tani 230,000 kwa mwaka, wakati uwezo wa viwanda kuzalisha kwa sasa ni tani milioni 2 kwa mwaka kama vitafanya kazi kwa asilimia 90 hadi 95.

Amesema uwezo wa kusindika mafuta umekuwa ni mkubwa kuliko uzalishaji wa zao hilo licha ya hamasa kubwa inayofanyika. Iringo alitaja sababu nyingine kuwa ni uhaba wa mbegu bora zinazotakiwa, akifafanua kuwa hali hiyo inapunguza uzalishaji.)

Ili kuokoa jahazi, Iringo alisema hakuna namna, zadi ya Watanzania kuwa wavumilifu hadi Mei na Juni ambako mavuno yataanza katika baadhi ya maeneo nchini, kwa kuwa si lazima mafuta kuagizwa nje.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kwa sasa bei ya alizeti sokoni haikamatiki kwa sababu gunia la kilo 100 linauzwa Sh70,000 hadi Sh80,000, kiwango ambacho anadai hakijawahi kufikiwa katika miaka ya nyuma kwani bei huwa kati ya Sh30,000 hadi Sh45,000. Katika Jiji la Dar es Salaam, mafuta ya alizeti ya ujazo wa lita tano yanauzwa kati ya Sh25,000 hadi Sh29,000 kutoka Sh19,000 miezi minne iliyopita.

Kwa upande wa mafuta yanayotoka nje ya nchi, dumu la lita 20 lililokuwa likiuzwa Sh50,000 hadi Sh55,000 sasa linauzwa kati ya Sh78,000 hadi Sh80,000.

Wakati huohuo, lita tano zinauzwa Sh22,000, lita tatu Sh14,500 na lita moja Sh5,500 kutoka Sh3,500.

Katika wilaya ya Sumbwanga mkoani Rukwa, bei ya mafuta ya alizeti imepaa kutoka Sh50,000 iliyozoeleka kwa lita 20 mpaka Sh90,000.
Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here