Mwakalebela: Rage ameshapitwa na wakati

0
Fredrick Mwakalebela

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amemjibu Mwenyejiti wa zamani wa Simba SC Ismail Aden Rage, kufuatia kauli yake aliyoitoa kuhusu sakata la kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison.

Mwakalebela alisema Rage, hana nafasi kwenye sakata hili, na taarifa aliyoitoa kwa kuutaka uongozi wa Yanga kuachana na kesi ya Morrison na kuendelea na mambo mengine haina mashiko.

Alisema mdau huyo ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha soka nchini (FAT), kwa sasa Shirikisho la soka (TFF), alishapitwa na wakati na endapo anataka kujua ukweli wa kesi ya mchezji huyo kama ipo CAS, amfuate muhusika.

“Rage ameshapitwa na wakati na kama anataka kujua ukweli wa kesi yetu na Morrison huko CAS, basi amfuate Mchezaji wake Morrison atamuonyesha Document (Nyaraka) zote na kila kinachoendelea,”alisema Mwakalebela.

Mwishoni mwa juma lililopita Mwakalebela alipozungumza na waandishi wa habari akiwa jijini Mbeya na kueleza kuwa, uongozi wa Yanga, unaamini kwamba haki yao ya mchezaji wao wa zamani Bernard Morrison itatendeka kwa kuwa kesi itasikilizwa baada ya FIFA kuwapa jaji atakayesikiliza kesi hiyo.

Ismail Aden Rage

Morrison, ambaye aliitumikia Yanga kwa takribani miezi sita msimu uliopita, alijiunga na Simba SC msimu huu 2020/21 ambapo usajili wake ulileta mvutano mkubwa kiasi cha kufikishana TFF, na baadae alishinda kesi iliyothibitisha yupo huru kujiunga na timu yoyote baada ya kubaini mapungufu kwenye mkataba wake.

Hivi karibuni, Rage alitoa ushauri huo kwa viongozi wa Yanga, baada ya Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Mwakalebela kutoa taarifa za maendeleo ya kesi ya Morisson alipozungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya.

Rage, alisema Yanga wanapaswa kuendelea na mambo mengine ya kimaendeleo ndani ya klabu yao, na kuachana kabisa na suala la kiungo huyo kutoka nchini Ghana, ambalo amedai litawapotezea muda.

Alisema hawawezi kupata chochote kile kupitia kesi hiyo, ambayo tayari imeshatolewa hukumu la Shirikisho la soka nchini TFF kupitia kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji chini ya mwenyekti wake Elias Mwanjala.

Hata hivyo, aliwataka viongozi wa Yanga kuionesha hadharani barua wanayodai wameipata kutoka CAS, ambayo inawathibitishia kesi ya Morisson imepokelewa na kupangiwa hakimu wa kuisikiliza.

Rage, alienda mbali zaidi kwa kusema, hakuna sheria yoyote ya CAS, inayotaka mshitaki na mshitakiwa walipe pesa ili kesi yao isikilizwe katika mahakama hiyo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here