Muhula wa pili wa JPM: Mazingira bora zaidi biashara, uwekezaji

  0

  Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

  SERIKALI ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Magufuli imeahidi kuwa katika kipindi chake cha pili mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji yatakuwa bora zaidi huku sekta binafsi ikipewa umuhimu wa pekee.

  Hii ni kutokana na kile alichoeleza Rais Dk. Magufuli wakati wa hotuba yake ya kufungua Bunge la 12 Novemba 13, 2020 kuwa pamekuwepo na urasimu mwingi na kusumbuliwa kwa wawekezaji kwa kuzungushwa na hivyo kuwafanya wakate tamaa.

  Rais Magufuli alisema ili kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, wataendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ikiwemo kuangalia masuala ya kodi na kuondoa vikwazo na urasimu.

  “Pamekuwepo na urasimu mwingi na kusumbuliwa kwa wawekezaji kwa kuzungushwa zungushwa na hivyo kuwafanya wakate tamaa. Mimi nataka mwekezaji mwenye fedha akija apate kibali ndani ya siku 14.,” alisema Rais Magufuli mbele ya wabunge na kutangaza kuhamisha suala la uwekezaji ikiwa ni pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ofisi ya Rais, “ ili hao wanaokwamisha nikapambane nao mwenyewe.”

  Nchi yetu pia imebarikiwa kuwa na maeneo mengi yanayofaa kwa shughuli za uvuvi, ikiwemo Ukanda wa Pwani, Maziwa, mito na mabwawa. Hali hii inafanya sekta hii kuwa na nafasi ya kutoa mchango mkubwa kwenye kukuza Pato la Taifa na pia kupambana na umasikini na tatizo la ajira.

  Hata hivyo, kwa sasa, mchango wake bado ni mdogo. Hivyo basi, kwenye miaka mitano ijayo tunakusudia kuikuza sekta hii, ikiwemo kuimarisha shughuli za uvuvi kwenye Bahari Kuu, ambako tumekuwa tukipoteza mapato mengi.

  Alisema , zaidi ya hapo, wamepanga kujenga Ukanda na Kongani (clusters) za viwanda kila mkoa kulingana na mazao na maliasili zinazopatikana.

  SEKTA BINAFSI KUPEWA UMUHIMU WA KIPEKEE

  “Hata hivyo, najua, ili kufikia malengo haya, tunategemea sana kupata ushirikiano kutoka sekta binafsi. Kama mnavyofahamu, sekta binafsi ndiyo injini ya kujenga uchumi wa kisasa,” alisema Rais Magufuli.

  “…katika kipindi cha miaka mitano ijayo, sekta binafsi itapewa umuhimu wa pekee sana. Tunataka mtu yeyote atakayetaka kuwekeza asisumbuliwe kwa kuwekewa vikwazo vya aina yoyote.

  Aliweka wazi kuwa Watanzania ni matajiri lakini baadhi yao wanasita kuwekeza hapa nchini kwa kuogopa kusumbuliwa “na maswali yasiyo na msingi. Tunahitaji kuwa na Mabilionea wengi wa Kitanzania. Nataka Watanzania wote washiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi yao. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania mnaonisikiliza, wakati wa kufanya mambo bila woga ni sasa.”

  Rais Magufuli pia alisema kwenye miaka mitano ijayo pia watafungua milango kwa sekta binafsi kufanya majadiliano na Serikali ili kutafuta mwafaka ya migogoro ya biashara (business disputes) iliyopo kwa faida ya pande zote mbili.

  “Lengo letu ni kuona Tanzania inakuwa mahali pazuri pa kufanya biashara duniani. Kwenye miaka mitano iliyopita, tumefuta tozo 168, ambapo 114 zitahusu kilimo, mifugo na uvuvi na tozo nyingine 54 za biashara.

  Magufuli pia alieleza mazingira mazuri yanazopatikana nchini kwa watu wanaotaka kuwekeza ikiwemo uwepo wa amani na utulivu na soko la kutosha la bidhaa.

  “Na napenda niwahakikishie watu wa sekta binafsi kuwa, Tanzania ni mahali pazuri na sahihi pa kuwekeza. Nchi yetu ina amani na utulivu; tumebarikiwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji; nchi yetu ipo kwenye eneo la kimkakati; sisi pia ni Wanachama wa jumuiya mbili, EAC na SADC, ambazo zina soko la watu takriban milioni 500.

  “Kwa hiyo narudia, kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza hapa nchini. Na kwa bahati nzuri, tangu mwaka jana, tumeanza kutetekeleza Mpango wetu wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini (yaani Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment in Tanzania). Hivyo basi, mazingira ya biashara na uwekezaji, kwenye miaka mitano ijayo, yanatarajiwa kuwa bora zaidi,” alisisitiza.

  Aidha Serikali imepanga kutoa vivutio maalum kwa watakaowekeza katika viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo .

  “Nitumie fursa hii, kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza bidhaa za mifugo (nyama, ngozi, maziwa, kwato, n.k.). Na katika hilo, tunaahidi kutoa vivutio maalum kwa watakaowekeza kwenye viwanda hivyo ambavyo vitasaidia kuinua vipato vya wafugaji wetu na pia kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania. Na hapa, nataka niweke bayana kuwa, watendaji watakaokwamisha ujenzi wa viwanda hivyo tutawashughulikia.”

  KUBORESHA MIUNDOMBINU

  Rais Magufuli alisema ili kukuza uchumi pamoja na sekta za uzalishaji ni lazima kuimarisha miundombinu, hususan ya usafiri na nishati ya umeme.

  “Kamwe, huwezi kukuza sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, uchimbaji madini na utalii bila kuimarisha miundombinu na huduma za usafiri pamoja na upatikanaji wa huduma za umeme. Kwa hiyo, kama ilivyokuwa kwenye miaka mitano iliyopita, tutaendelea kuweka mkazo mkubwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya usafiri na kuboresha huduma za usafirishaji,” alisisitiza.

  LEAVE A REPLY

  Please enter your comment!
  Please enter your name here