Mshauri wa Yanga Senzo Mazingiza ahojiwa polisi

0

NA MWANDISHI WETU

ALIYEKUWA Mtedaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Senzo Mazingiza ameitwa kituo cha  Polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam jana, kufanyiwa mahojiano kisha na kuachiwa.

Ikumbukwe kwa sasa Mazingiza ni mshauri mkuu ndani ya Klabu ya Yanga kwenye mchakato wa kuelekea mabadiliko ambapo aliibukia huko muda mfupi baada ya kubwaga manyanga ndani ya Simba.

Akizungumza na JAMVI LA HABARI, Kamanda wa Polisi Kinondoni, Edward Bukombe , alisema ni kweli Mazingiza alifika kituoni hapo lakini badae aliondoka.

“Mbona hayupo kwenye kituo cha polisi aliishaachiwa muda mrefu, kuna kipindi alihojiwa halafu akaachiwa, hayupo tena.

“Kuhusu sababu za kufanyiwa mahojiano bado sijapata taarifa rasmi kwa sababu alikuwa anashughulika na vijana wangu,”alisema Kamanda Bukombe.

Hivi karibuni baada ya klabu ya Simba kufanya vibaya ziliibuka taarifa zinazodai kwamba Mazingiza alikuwa akifanya vitendo vya kuihujumu klabu hiyo, kwa kushirikiana na Hashim Mbaga, aliyekuwa mkurugenzi wa mashabiki na wanachama wa Simba ambaye naye alifutwa kazi.

Chini ya Kocha Mkuu Sven Vandenbroeck, Simba ilipokea vichapo kwenye mechi mbili mfululizo na kuyeyusha pointi sita ambapo ilikuwa dhidi ya Tanzania Prisons ilipopoteza kwa kufungwa bao 1-0 kisha ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.

Kutokana na matokeo hayo mabovu Simba ilifanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi kwa kumuondoa Mohamed Mwarami aliyekuwa kocha wa makipa pamoja na Patrick Rweyemamu ambaye alikuwa ni Meneja wa Simba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here