Mpiga kura anaweza kuomba karatasi nyingine akikosea au kubadili maamuzi

0

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa ufafanuzi wa utaratibu wa upigaji kura katika uchaguzi mkuu na kusema mpiga kura aliyeharibu kwa bahati mbaya karatasi ya kupigia kura akiwa kwenye kituturi kwenye kituo cha kupigia kura, anaweza kuirudisha karatasi hiyo kwa msimamizi wa kituo na kuomba apewe nyingine ili apige kura yake vizuri.

Hayo yalisemwa na Ofisa wa NEC, Flora Mkama jijini Dar es Salaam jana wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari watakaoripoti uchaguzi mkuu unaofanyika nchini kote wiki ijayo Oktoba 28.

Akitoa mada kuhusu utaratibu wa kupiga kura, Mkama alisema mpiga kura aliyefika kituo cha kupigia kura na kuhakikiwa kisha kupewa karatasi ya kupigia kura na kuelekea kwenye kituturi cha kupigia na baadae akabaini amekosea kupiga anaruhusiwa kumrudishia msimamizi wa kituo karatasi hiyo kabla ya kuitumbukiza kwenye boksi la kura na kuomba nyingine ili kukamilisha upigaji kura wake.

“Inawezekana wapiga kura hawajui kuwa wana haki ya kuomba karatasi nyingine ya kupigia kura endapo itatokea kwa bahati mbaya amekosea au amebadili uamuzi wake wakati akiwa kwenye kituturi atarudisha karatasi hizo kama ni zote au moja kati ya hizo tatu, yaani rais, ubunge au udiwani na kuomba kupewa nyingine ili akachague mgombea amtakaye.”

“Inawezekana mtu amekosea katika kuchagua akakuta ameweka alama kwa mgombea ambaye hakumtaka au ameamua kubadilisha uamuzi sasa kuliko aharibu ile karatasi kwa kukatakata anatakiwa airudishe kwa msimamizi alafu aombe nyingine akapige,” alisema.

Mkama alisema mpiga kura akiirudisha karatasi hiyo kwa msimamizi wa kituo msimamizi huyo ataichukua na kuandika kwa nyuma ‘Imefutwa’ na kuiweka katika bahasha namba 3A iwapo ni ya Rais au kama ni ya wabunge itawekwa bahasha namba 3B na udiwani bahasha namba 3 C.

Alisema mpiga kura atakayepewa karatasi nyingine ya kupigia kura ni yle tu ambaye alikuwa kwenye kituturi cha kupigia kura na sio aliyekwishapiga kura na kutumbukiza kwenye sanduku la kura.

Akizungumzia wapiga kura wenye sifa, Mkama alisema wanaoruhusiwa kupiga kura kwenye kituo husika ni wale tu waliojiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura kwenye kituo hicho.

Aidha, alisema waliopoteza kadi ya mpiga kura lakini wana vitambulisho vingine vilivyoruhusiwa na tume kutumika wanaweza kupiga kura baada ya kuhakikiwa.

Hata hivyo, aliwataka wapiga kura kufuata maelekezo ya msimamizi wa kituo na kuepuka kukiuka taratibu za uchaguzi ili kuepusha migogoro isiyo na sababu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here