Mmoja afariki, wanane walazwa kula mzoga nguruwe pori

0

NA MWANDISHI WETU, KATAVI

MTU mmoja Katarina Zebedayo (38) mkazi wa kijiji cha Kabanga Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika amefariki dunia huku watu wengine wanane wakilazwa baada ya kula nyama ya mzoga wa nguruwe pori.

Akizungumza jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga amesema tukio hilo lilitokea Desemba 7, 2020 jioni na kwamba watu hao wanane walipatiwa matibabu katika kituo cha afya Mishamo.

Amesema wananchi waliona mzoga wa mnyama huyo katika mashamba yao, “waliuchukua na kumchuna ngozi kisha wakagawana nyama ambayo waliipeleka majumbani mwao na kuila.”

Amesema muda mfupi baada ya kula nyama hiyo walianza kuumwa tumbo lakini badala ya kwenda hospitali walianza kunywa dawa za kienyeji na Desemba 10 Katarina alifariki dunia akiwa nyumbani kwake.

Alisema baada ya kifo hicho, baadhi ya waliokula nyama hiyo walitoa taarifa kwa ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Theodoli Philipo.

“Ndipo walipobaini kuwa watu wanane, sita wakiwa watoto walikula nyama hiyo na wanaugulia majumbani. Walichukuliwa hadi kituo cha afya Mishamo kupatiwa matibabu zaidi,” alisema kamanda huyo.

Aliwataja wanaoendelea kupewa matibabu kuwa ni Leonard Kabula (17), Sifa Kabula (4), Levis Kabula (3), Boniphace Kabula (1), Seth Eliya (30), Lidnes Mayokolo (9), Noadia Balasiano (36), na Sostenes Philipp (1).

“Hali zao zinaendelea vizuri lakini uchunguzi tulioufanya eneo la tukio hakuna mabaki yoyote ya mnyama huyo, wahanga walitupa nyama na mabaki yote chooni baada ya kuona wanapata madhara,” alisema Kuzaga

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here