Mkenya, Anthony Akumu aitamani Yanga

0

NA MWANDISHI WETU

KIUNGO wa timu ya Kaizer Chiefs, Mkenya, Anthony Akumu, ameibuka na kusema kuwa hana tatizo lolote ikiwa atahitajika katika kikosi cha Yanga kwa kuwa yeye anachoangalia ni suala la masilahi mazuri kwake.

Akumu alitoa kauli hiyo baada ya Mjumbe wa Kamati ya Usajili Yanga na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wao, Injinia Hersi Said, kuweka picha ya kiungo huyo katika ukurasa wake wa Instagram kwa lengo la kumtakia heri ya siku yake ya kuzaliwa.

Kitendo cha Hersi kuweka picha ya kiungo huyo kwenye akaunti yake ya Instagram na kumtakia heri ya kuzaliwa, kimeibua maswali mengi na wadau wengi wameona kama Yanga wanaelekea kumsajili nyota huyo.

Kiungo huyo alianzia kucheza soka akiwa katika Klabu ya Gor Mahia kisha akatimkia Al Khartoum ya Sudan kabla ya kujiunga na Zesco United ya Zambia na mapema mwaka huu akajiunga na Kaizer Chiefs akichukua nafasi ya aliyekuwa kiungo wa Simba, James Kotei, baada ya kushindwa kupata nafasi kwenye timu hiyo.

Akizungumza jijini mara baada ya picha hiyo katika kuonekana kwenye ukurasa wa Injinia Hersi, Akumu alisema kuwa kwa upande wake hana shida yoyote ikitokea kuhitajika na Yanga kupitia kiongozi hiyo kwani upande wake hatakuwa na wasiwasi kwani anajuana naye vizuri.

“Yule ninamfahamu vizuri, sina shida kama atanipa ofa ya kuja Yanga, kitu kikubwa ni kusikilizana katika suala la masilahi kwa sababu sitaki kubaki hapa kwa muda mrefu.
“Unajua ligi ya Afrika Kusini ni kubwa lakini hata timu niliyopo pia ni kubwa lakini haiwezi kuwa sababu ya kushindwa kwenda sehemu nyingine ikiwa itakuja ofa kubwa kwangu,” alisema Akumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here