Mike Gidion: Gavana wa ‘bling bling’

0

NAIROBI,KENYA

MIKE Gidion Kioko Mbuvi Sonko, kama alivyojulikana na wengi, hakuwa Gavana wako wa kawaida. Tofauti na wanasiasa wengi wanaojulikana kwa kuvaa suti za bei ghali, Sonko, mwenye umri wa miaka 45, alikuwa na ujana ndani yake.

Bunge la Seneti nchini Kenya limepiga kura kumuondoa Mike Mubuvi Sonko kama gavana wa Nairobi , katika hatua ambayo imekomesha miaka mitatu ya utawala wake uliogubikwa na utata.

Sonko anatuhumiwa kwa uvunjaji wa katiba, matumizi mbaya wa mamlaka , utovu wa nidhamu, na uhalifu.Mara kwa mara Sonko alionekana katika maeneo ya umma akiwa amevalia mavazi ya wanamitindo wa Marekani kama vile Gucci na Louis Vuitton.

Anajulikana sana kwa kuvaa vito vya thamani; pete na bangili nyingi za dhahabu, ambavyo vinaja hasa wa Nairobi huviita ‘bling bling’.

Sonko alipata umaarufu mkubwa alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kama Mbunge wa eneo bunge la Makadara jijini Nairobi. Mara moja alianza kuonekana katika maeneo ya umma akisambaza pesa kwa watu maskini hususan katika maeneo ya nyumba za za vibanda.

Umaarufu wake uliendelea kupanda zaidi na zaidi baada ya kwenda katika mitaa ya mabanda ya Mukuru, na kulała nje usiku kucha na wakazi wa huko waliokuwa wamebomolewa nyumba zao na serikali.

Sonko alianzisha mradi wake maarufu kama ‘Sonko Rescue Team’ ambao uliwasaidia wakazi wa mitaa ya mabanda wakati wa harusi, kutoa magari ya kusafirisha miili ya wapendwa wao waliofariki, magari ya zima moto, ambilansi na hata kusafisha maeneo kadhaa jiji la Nairobi.

Lakini kando na hayo mazuri, Gavana Sonko atakumbukwa kwa rekodi ya uhalifu. Idara ya magereza nchini Kenya inasema Sonko alitoroka gerezani takriban miaka 20 iliyopita.

Ni madai ambayo Sonko mwenyewe aliyathibitisha katika mahojiano ya Televisheni nchini Kenya.Mwaka jana Sonko pia alikamatwa kwa tuhuma za ufisadi, japo amesisitiza kuwa tuhuma hizo zilikuwa njama za wapinzani wake kisiasa.

Sonko anakumbukwa sana kwa kutumia lugha chafu, na maneno yasiyoweza kuchapishwa, hususan wakati alipokuwa akilumbana na wapinzani wake wa kisiasa na vyombo vya habari nchini humo.

Wakati wa kesi ya kumvua Ugavana, vikao vya Bunge la Seneti nusra visitishwe pale kanda moja ya sauti ya Sonko ilipochezwa, akifoka kwa matusi mazito.

Mapema mwaka huu, Sonko aligonga vichwa vya habari vya kimataifa alipopoweka chupa ndogo za mvinyo wa Hennessy kwenye kifurushi cha kuwasaidia maskini wakati wa makali ya virusi vya corona.

Wakati huo Sonko alitetea uamuzi huo, akisema pombe kidogo itakata makali ya Corona mwilini.

Hadi wakati akitimuliwa ofisini, Sonko amekuwa kipenzi cha wengi, hususan miongoni mwa watu masikini.

Lakini wale wasiokubaliana na sera zake wanamkosoa kwa ukali, wakidai hakuwa na hadhi wala maadili ya kuwa kiongozi.

Na sasa baada ya Sonko kutimuliwa ofisini jana, Spika wa bunge la Nairobi, Benson Mutura, anachukua madaraka kama Kaimu Gavana hadi pale uchaguzi mdogo utakapofanywa katika muda wa siku 60.

Sasa je, Sonko ndiye jiwe la pembeni lililokataliwa na wajenzi? Au je, yeye ni mbwa mwitu aliyejifunika kwa ngozi ya kondoo? Ni muda tu unaweza kujibu maswali hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here